Bidhaa bandia zaundiwa mkakati

Muktasari:

Ili kufanikisha mpango wa kuwa na nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025, Serikali imesema itaendelea kupambana kwa nguvu na bidhaa bandia kwakuwa zinadumaza maendeleo ya viwanda na uwekezaji.

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia ili viwanda vya ndani viweze kushamiri kama sehemu ya mpango wa Serikali wa kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Edwin Mhende leo Alhamisi Aprili 25 wakati wa semina ya udhibiti wa bidhaa bandia iliyoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC) kwa wamiliki wa viwanda mkoani Dar es Salaam.

"Bidhaa bandia zinaathiri mfumo mzima wa ukuaji wa uchumi wa soko na maendeleo ya viwanda kwasababu humuondoa kwenye soko mfanyabiashara na mmliki halisi hivyo mapambano yake ni jambo la watu wote hususan Serikali na wamiliki wa viwanda," amesema.

 Dk Mhende Amesema kuna changamoto ya kuongezeka kwa bidhaa bandia (bila kutaja takwimu) hivyo amewataka wamiliki wa viwanda kusajili alama za bidhaa zao ili ziweze kujulikana sokoni jambo litakalo kuza viwanda na kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na nchi ya viwanda. Mkibaini bidhaa bandia toeni taarifa haraka ili tuweze kuchukua hatua stahiki," amesema.

Naye mkurugenzi mtendaji wa FCC, Dk John Mduma amesema tume hiyo inapambana na bidhaa hizo kwa nguvu kwani hudumaza maendeleo ya viwanda na kusababisha hasara kwa wamiliki ambao wameitikia wito wa kujenga viwanda.

"Kutokana na kukua kwa teknolojia kumekuwa na ongezeko la bidhaa bandia nchini na duniani, hii ni kutokana na urahisi wa kuiga nembo na alama za biashara ndiyo maana tumeongeza juhudi za utoaji wa elimu kwa wadau wote," amesema.

Dk Mduma amesema mwananchi anaponunua bidhaa bandia hawezi kupata ufumbuzi kwa urahisi hususan pale anapotakiwa kufidiwa bidhaa husika inapomsababishia madhara.

Mtaalamu wa sera za biashara kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) ambaye alihudhuria semina hiyo, Frank Dala amesema bidhaa bandia ni changamoto kubwa kwa wazalishaji nchini na katika utafiti walioufanya walibaini elimu kwa walaji na wazalishaji ndiyo suluhisho la tatizo hili.