Bima kuanza kufidia mazao ya wakulima

Thursday February 14 2019

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) akiandika

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) akiandika maoni yaliyokuwa yakitolewa katika mkutano wa bima kwa majanga ya kilimo baada ya kuufunguzi mkutano huo katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), jijini Dar es Salaam.  Picha na Mathias Canal 

By Gadiosa Lamtey, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ili kumnusuru mkulima na hasara, Serikali inakamilisha sera ya bima ya Taifa itakayojumuisha sekta hiyo.

Mpango huo umeelezwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga kuwa ni mkakati wa Serikali kuvitafutia suluhisho la kudumu vikwazo vilivyopo ambavyo vinazorotesha kilimo na kumpunja mapato anayostahili.

“Mpaka Juni, orodha ya mazao itakuwa inapatikana ili kuzisaidia kampuni za bima kuangalia mazao yapi waanze nayo na nimemwagiza kamishna wa bima kuharakisha mchakato wa uandaaji sera ili kuiwasilisha serikalini kwa hatua nyingine,” alisema Waziri Hasunga.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Hasunga alisema Serikali inaandaa kanzidata au taarifa ya mazao yote ya kipaumbele ili kuziruhusu kampuni nyingi zaidi kuwahudumia wakulima.

Kati ya kampuni 29 za bima zilizopo, ni chini ya tano zinatoa bima ya kilimo.

Akizungumzia mkakati huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware alisema wanafanya kazi kwa kushirikiana na wadau muhimu kuhusu kuanza kuwafidia wakulima.

Alisema utaratibu ukikamilika, wakulima watafidiwa kwa mfumo unaotumika kwingineko duniani.

Sekta ya kilimo nchini ni muhimu kwa mambo mawili makuu, kuhakikisha uhakika wa chakula na pili ni kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Taarifa ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa mwaka 2018/19, Tanzania ilikuwa na tani 95,534 za akiba ya chakula huku ikipunguza uagizaji kutoka nje.

Ripoti hiyo inasema, Desemba mwaka jana, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ilishuka kwa asilimia 3.2 na kufika Dola 8.38 bilioni za Marekani ikilinganishwa na Dola 1.02 bilioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.

Kushuka kwa mauzo hayo, BoT inasema: “Kulitokana na kushuka kwa mauzo ya chai, korosho na karafuu. Mapato ya korosho yamepungua kutokana na kuchelewa kwa usafarishaji wa zao hilo kulikochangiwa na bei ndogo.”

Advertisement