Bomoabomoa nyingine Dar es Salaam

Thursday March 14 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu bomoabomoa iliyofanyika Kibamba hadi Kimara jijini Dar es Salaam imalizike, nyingine inatarajia kupiga hodi wilayani Kigamboni ambako inalenga nyumba za watu waliojenga lilipo bomba la mafuta la Tazama.

Wakazi wa manispaa hiyo watakaoathirika ni wale waliojenga eneo lilipopita bomba hilo kata za Tumbi, Mjimwema na Vijibweni. Hata hivyo haijafahamika idadi ya nyumba zitakazoathirika.

Mbali ya waliojenga jirani, pia bomoabomoa hiyo itawakumba waliojenga nyumba zao juu ya bomba hilo. Nyumba zilizo hatarini kubomolewa ni zile zilizojengwa baada ya upembuzi wa mradi wa awali uliokuwa ukijulikana kama Kigamboni City.

Akizungumza kwenye mkutano wa kukusanya maoni kwa wananchi ulioandaliwa na Manispaa ya Kigamboni kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo Jumuishi (I4ID) jana, mwakilishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Toby Rejea alisema ramani ya eneo hilo ipo na wananchi wanaweza kwenda kuiangalia katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ili kujiridhisha.

“Waliojenga na wanaoendelea kujenga kwenye maeneo haya wanapaswa kuondoka kwa sababu eneo hilo ni hatarishi kwa maisha yao,” alisema Rejea.

Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Maabadi Hoja alisema pamoja na mchakato huo kuwa na lengo la kufahamu upungufu uliopo katika mpango wa uendelezwaji wa mji huo, pia unatoa tahadhari kwa watu wanaoishi katika maeneo ilipo miradi kinyume na utaratibu wakiwamo waliojenga ndani ya eneo linakopita bomba hilo.

Alisema yapo maeneo yaliyovamiwa ambapo wahusika wanapaswa kuondoka.

“Waliokutwa na bomba watavunjiwa na watalipwa, ila waliojenga (jirani na bomba) baada ya bomba kuwekwa watavunjiwa kwa hasara kwa sababu tulishatangaza (wasijenge), lakini wao wakakaidi,” alisema.

Awali, akifungua mkutano huo, mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri alisema utaratibu wa kukusanya maoni kwa wananchi umefanyika baada ya kutokea makosa mbalimbali katika mpango wa kupanga mji huo uliowasilishwa miaka sita iliyopita.

“Upo upungufu mbalimbali unaoufanya mpango kamambe wa Jiji la Dar es Salaam usikidhi matakwa ya wana Kigamboni, upo upungufu wa kisheria, kitakwimu, kitaalamu na kiusalama na baada ya kushauriana na washauri elekezi wa mpango huo, Kigamboni kupitia wananchi wake imepewa fursa ya kuboresha,” alisema Sarah.

Advertisement