Chadema wakana tuhuma vitambulisho

Sumbawanga. Uongozi wa Chadema mkoa wa Rukwa umekana madai ya kwamba wao ndio kikwazo cha wajasiriamali kutochukua vitambulisho vilivyotolewa na RaisJohn Magufuli kwa wafanyabiashara wadogo.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila amesema hayo baada ya kuwapo kwa madai kwamba wamekuwa wakishawishi wafanyabiashara wadogo wasichukue vitambulisho hivyo kwa madai ni mpango wa Serikali wa kuchukua takwimu ili waweze kusajiliwa TRA ili waanze kulipa kodi.

“Tuhuma hizi zinazoelekezwa kwetu si za kweli ila kilichopo ni uongozi wa manispaa wameshindwa mbinu za kuwashawishi wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kujitokeza kuchukua vitambulisho hivyo kutokana na mwamko mdogo tofauti na matarajio ya Serikali,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, Jacob Mtalitinya amemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa hali imekuwa tofauti na matarajio kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo propaganda za kisiasa.