Chaguzi ndogo tatu zatumia Sh12 bilioni

Muktasari:

  • Chaguzi hizo tatu za Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli zilifanyika Septemba 2018 na miongoni mwa matumizi ya fedha hizo ni Sh3.7 bilioni zilizotumika kama posho maalum pamoja na Sh16.5 milioni zilizotumika kwa ukarimu.

Dar es Salaam. Uchaguzi wa marudio uliofanyika katika majimbo matatu, umegharimu zaidi ya Sh12 bilioni hivyo kuthibitisha haja ya kubadili mfumo wa kutekeleza demokrasia nchini kama baadhi ya wadau wanavyopendekeza.

Taarifa ya Serikali ya mabadiliko ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2018/19 inaonyesha kiasi hicho kilitumika kufanikisha uchaguzi wa marudio katika majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli uliofanyika Septemba 16, 2018.

Taarifa hiyo inayoonyesha mabadiliko ya matumizi mpaka Desemba 2018 inabainisha kuwa Hazina ilipeleka zaidi ya Sh12.44 bilioni ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanikisha marudio hayo.

Kwenye mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo, kiasi kikubwa zaidi kilielekezwa kwenye posho maalumu ambako Sh3.71 bilioni zilitumika huku Sh2.08 bilioni zikiwawezesha watumishi wa tume hiyo kujikimu (perdiem) kwa siku 30 za kusimamia uchaguzi huo.

Kwa kuwa uchaguzi huo uliwapa majukumu ya ziada, Sh1.24 bilioni zilitumika kuwalipa watumishi wa tume ukiacha Sh917.16 milioni kwa ajili ya usafiri wakiwa kwenye majimbo hayo huku chakula na viburudisho kwa muda wote wa mchakato huo vikigharimu Sh626.21 milioni.

Tume ilitumia Sh1.22 bilioni kuchapisha na kudurufu nyaraka muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo huku ikiajiri vibarua waliolipwa Sh105.91 milioni. Kufanikisha mpango mzima, wajumbe wote walilipwa Sh228.41 milioni kama posho ya vikao walivyohudhuria.

Ili kupumzika, malazi ya watumishi wa tume yaligharimu Sh306.35 milioni huku wakikodi magari binafsi kwa Sh291.7 milioni. Dizeli Sh548.866 milioni ilinunuliwa na Sh32.4 milioni zikinunua vocha kwa ajili ya mawasiliano ya simu.

Kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, tume ilikodi maturubali na vifaa vya kupigia kambi kwa Sh258.27 milioni huku ikitumia Sh24.19 milioni kuwasafirisha watendaji wake kwa ndege.

Fedha nyingine zilitumika kwa ukarimu (Sh16.45 milioni), vifaa vya ofisi (Sh117.05 milioni), kompyuta na vifaa vyake (Sh72.84 milioni), matangazo (Sh145 milioni), huduma za mzabuni (Sh311.31 milioni) na mikutano ikigharimu Sh177.8 milioni.

Mkurugenzi wa uchaguzi, Athuman Kihamia alipoulizwa kwa simu alisema hayupo katika mazingira mazuri kuzungumza.

“Hebu nipigie baadaye, nipo kwa daktari hapa,” alisema.

Wakati NEC ikitumia fedha hizo, mgombea ubunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava alipita bila kupingwa.

Wadau

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee amesema licha ya taarifa hiyo kuonyesha fedha hizo zilitumika katika majimbo matatu, lakini kiuhalisia ni mawili kwani Korogwe Vijijini haukufanyika kwa kuwa mgombea wa CCM alipita bila kupingwa.

“Mgombea wa Chadema alifika kwa wakati lakini fomu yake haikupokelewa. Kwa hiyo uchaguzi ulifanyika kwenye majimbo mawili tu hivyo kila mmoja ulitumia zaidi ya Sh6 bilioni,” alisema Mdee.

Maoni ya Mdee ambaye ni waziri kivuli wa fedha na mipango yanafanana na ya Mbunge wa Kilwa Kusini, Said Bungara maarufu kama Bwege aliyesema hakukuwa na sababu za msingi kufanya uchaguzi.

“Kama mbunge anahama tu chama, fedha nyingi zinatumika za nini? Huo ni ufujaji kwa masilahi ya CCM,” alisema na kuongeza,

Hata hivyo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema suala la gharama katika demokrasia haliepukiki.

“Tusingefanya uchaguzi tungewapataje hao wawakilishi? Kuna wakati tulisema tubadili huu mfumo lakini wapinzani wakaona tunakandamiza demokrasia,” alisema Lusinde.

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Profesa Ruth Meena alisema demokrasia ina gharama zake lakini suala la uchaguzi wa marudio linapaswa kuangaliwa.

“Tuangalie njia mbadala ya kufanya uchaguzi wa marudio, anaweza kuchukuliwa aliyeshika nafasi ya pili au vinginevyo,” alisema Profesa Meena.