Chemba katikati ya changamoto lukuki za elimu

Thursday March 14 2019

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Muungano

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Muungano iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba wakijisomea katika darasa chakavu, wakati wa mvua huwa ni kizungum-kuti. Picha na Ephrahim Bahemu 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2018, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilishika nafasi ya mwisho kitaifa kati ya halmashauri 186 ikiwa imeshuka kwa nafasi saba, kutoka 179 iliyoshika mwaka 2017.

Halmashauri hiyo pia ilishuka kwa nafasi saba mwaka 2016 kutoka 172 hadi 179 mwaka 2017.

Mwaka 2018 katika wilaya hiyo jumla ya wanafunzi 5,158 walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba, lakini kati yao waliofaulu kuendelea na masomo ya sekondari ni asilimia 37 tu.

Kutokana na matokeo hayo hafifu, Mwananchi lilifunga safari kwenda katika halmashauri hiyo ili kubaini changamoto zilizopo hadi kuifanya iwe ya mwisho.

Kaimu ofisa elimu ya msingi wa Chemba, Maenda Chambuko anasema changamoto ya ufaulu katika halmashauri hiyo ni uhaba wa miundombinu rafiki ya kufundishia na kujifunzia lakini kubwa zaidi ni upungufu wa walimu.

Anasema katika halmashauri hiyo kuna shule za msingi 103 zenye wanafunzi zaidi 65,120, lakini walimu waliopo ni 820 tu licha ya kuwa wanahitajika walimu zaidi ya 1,628, hivyo kuna upungufu wa walimu 808 kwa kuzingatia uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.

Kwa Chemba uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 79.4.

Chambuko anasema katika halmashauri hiyo changa kulikuwa na walimu wachache lakini waliendelea kuwa wachache kutokana na baadhi yao kustaafu na wengine, kufariki na kuondolewa kwa sababu ya vyeti feki. Ingawa Serikali iliongeza walimu 73, lakini walimu takribani 10 wanatarajiwa kustaafu mwaka huu.

“Kama unavyojua walimu wakiwa wachache ufundishaji unakuwa hafifu, mada hazimaliziki kama inavyopaswa wala hazifundishwi ipaswavyo. Tumeweka mikakati kadhaa ambayo itatutoa hapa tulipo,” anasema Chambuko.

Ukiachilia mbali changamoto ya walimu, halmashauri hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na samani kwa ajili ya kurahisisha mazingira ya kujifunza na kufundishia.

Chambuko anasema katika shule 103 za msingi zilizopo wilayani Chemba zina madarasa 731 huku yanayohitajika yakiwa ni 1,647, hivyo kuna upungufu wa madarasa zaidi 815.

Madawati nayo hayatoshelezi kwani yanayohitajika ni 17,506 lakini yaliyopo ni 16,178 hivyo upungufu ni madawati 1,328.

Kwa upande wa vyoo shule zote 103 zina matundu ya vyoo 941 kati ya 2,458 yanayohitajika.

Pia, kuna upungufu wa nyumba za walimu ambazo ni motisha kwa walimu kuishi maeneo yaliyo karibu na shule wanazofundisha ambapo kwa Chemba kuna nyumba 301 wakati zinazohitajika ni 1,647 hivyo kuna upungufu wa nyumba 1,224.

Kadhalika ofisi za walimu nazo hazitoshi kwani zilizopo ni 120 kati ya 243 zinazohitajika, hivyo kuna upungufu wa ofisi 123. Mbali na hivyo, kuna upungufu wa viti vya walimu, meza zao na makabati ya ofisi hizo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muungano, Emilian Malamsha anasema shule yake ina changamoto ya walimu na miundombinu.

Anasema ana walimu wanne huku wanafunzi wakiwa 310, vyumba vya madarasa vilivyopo ni vitatu, hivyo kulazimu wanafunzi kusoma kwa zamu na wengine kuchanganywa katika darasa moja.

“Darasa la kwanza na la pili wanasomea darasa moja wana ‘shift’ (wanapishana) asubuhi na mchana, darasa la tatu na la nne darasa moja, darasa la sita na saba darasa moja. Darasa la tano ndio hao wanaokaa kwenye chumba hicho ambacho hakijaezekwa jua likiwaka wanahamia chini ya mti,” anasema Malamsha huku akimuonyesha mwandishi wa habari chumba hicho.

Anasema wastani wa walimu katika shule hiyo hufundisha masomo 15 kwa wiki na yeye licha ya majukumu aliyonayo kama mwalimu mkuu lakini anafundisha vipindi saba.

Anasema vyoo viko sita vilivyogawanywa kwa usawa kati ya wavulana na wasichana na hakuna nyumba ya mwalimu.

Mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini anayefundisha katika shule mojawapo katika Tarafa ya Kwamtoro, anasema suala la uchache wa walimu ndiyo sababu kubwa kwa Chemba kufanya vibaya katika mitihani.

Anasema katika shule anayofundisha mwaka huu darasa la kwanza wapo zaidi ya wanafunzi 200, lakini wana mwalimu mmoja tu ambaye baada ya hapo anatakiwa afundishe na darasa la pili.

“Katika mazingira kama hayo wanafunzi wanajikuta hawafundishwi kwa muda unaostahili kutokana na walimu kuelemewa na majukumu mengi. Huku ni kawaida kukuta mtoto wa darasa la nne au la tano hafahamu KKK (kusoma, kuhesabu na kuandika),” anasema mwalimu huyo.

Katibu wa Chama cha Walimu Chemba, Zacharia Barajid anasema kuna upungufu wa walimu katika halmashauri hiyo na kuondolewa kwa walimu hewa kulipunguza morali ya kazi kwa kuwa mchakato wake ulichukua muda mrefu huku stahiki nyingine zikikwama.

Mikakati

Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo kupitia idara ya elimu ni pamoja na kutumia mpango wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) na taasisi ya Equip kutatua changamoto za miundombinu zilizopo katika sekta ya elimu.

Pia, halmashauri imepanga kuhakikisha wanafunzi katika shule zote wanapata chakula cha mchana (mpaka sasa shule 10 zimeanzisha mpango huo) pia wamepanga kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri na kushughulikia kwa haraka changamoto za shule na maslahi ya walimu.

Chambuko anasema tayari halmashauri imeimarisha uongozi katika shule mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubadili walimu wakuu sanjari na kuweka huduma maalumu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu ili kurahisisha mazingira ya kujifunza.

Tamisemi

Naibu Waziri wa Tamiseni, Mwita Waitara anasema halmashuri hiyo inapaswa kutumia mapato yake ya ndani kutatua baadhi ya changamoto kwa kuwa asilimia 40 ya mapato yanabaki katika halmashauri kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwamo elimu.

Advertisement