China yakwea kileleni uwekezaji nchini, yaipiku Uingereza

Thursday May 16 2019

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe 

By John Namkwahe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya miaka mingi ya ushawishi, uwekezaji kutoka China umezipiku nchi nyingine zinazovutiwa na fursa zilizopo nchini.

Miaka minane iliyopita, China ilikuwa inashika nafasi ya sita wakati Uingereza, Marekani, Afrika Kusini na Kenya zikiongoza orodha ya nchi zenye miradi yenye thamani kubwa nchini.

Akizungumzia hali hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe alisema Wachina wana desturi ya kuwekeza kwenye maeneo tofauti ya uchumi ikiwamo viwanda, kilimo, miundombinu na biashara.

Kwenye orodha hiyo ya sasa, Uingereza inashika nafasi ya pili kutokana na miradi yake yenye thamani ya Dola 5.54 bilioni za Marekani, ikifuatiwa na Marekani (Dola 4.7 bilioni), Mauritius (Dola 4.308 bilioni) na India Dola 2.2 bilioni.

Katika hotuba aliyoitoa Novemba 2012 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bomba la gesi asilia lenye thamani ya Dola 1.225 bilioni za Marekani, aliyekuwa balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema Tanzania ni miongoni mwa vitovu muhimu vya biashara kwa taifa hilo la Bara Asia.

Mwaka 2014, Afrika Mashariki ilichukua asilimia 16.3 ya uwekezaji wote uliofanywa na China barani Afrika.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisema ofisi yake inahaha usiku na mchana kuhakikisha wawekezaji wengi zaidi wanakuja nchini. “Tunakutana na wafanyabiashara wakubwa wa China na kuwaeleza fursa tulizonazo. Inapobidi tunawaalika waje nyumbani kujionea fursa wanazoweza kuzitumia. Wafanyabiashara wetu pia wanapata nafasi ya kuja kuonyesha bidhaa zao na kuingia mikataba ya soko la hapa,” alisema Kairuki.

Licha ya mikutano ya kuvutia wawekezaji kuja nchini, ubalozi wa Tanzania nchini China umefanikisha safari kadhaa za wawekezaji kutembelea nchini ndani ya miaka mitatu iliyopita. Safari ya hivi karibuni ni ya watalii zaidi ya 340 wanaojumuisha waandishi wa habari, wafanyabiashara na wasanii.

Advertisement