DC: Marufuku dini kufundishwa usiku

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pascas Muragili

Muktasari:

Hatua hiyo imetokana na diwani kulalamikia walimu wa madrasa

Singida. Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pascas Muragili amepiga marufuku wanafunzi wa elimu ya dini ya Kiislamu kwenye madrasa kusoma nyakati za usiku hadi saa sita kwa kuwa kunahatarisha usalama wao na kuchangia momonyoko wa maadili.

Marufuku hiyo ilitolewa juzi baada ya diwani wa Ughandi, Itiege Rajabu Issa kueleza kwenye kikao cha ushauri wilaya kuwa kuna maeneo katika jimbo la Singida Kaskazini wanafunzi wanafundishwa Quran, kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 6:00.usiku.

Issa alisema nyakati hizo licha ya kuhatarisha usalama wa wanafunzi, inachangia kushuka kwa taaluma kutokana na wanafunzi wa kike hubakwa huku wa kiume wakijiingiza kwenye vitendo vya ngono.

“Mwanafunzi ambaye hadi saa 6:00 usiku hajalala ina maana akiingia darasani lazima alemewe na usingizi. Hivyo, atalala tu kwa ujumla usikivu wake utakuwa duni hatari ni kwamba mbele ya safari tutakuwa tunazalisha mbumbumbu,” alisema Issa.

Hata hivyo, Sheikh wa Kata ya Merya, Ramadhani Dahiya alipinga kutekelezwa kwa marufuku hiyo kwa kuwa ni kwenda kinyumme na taratibu za dini ya Kiislamu.

“Dini yetu inatuelekeza kila muumini akakikishe anapata elimu dunia na ya dini sambamba. Wanafunzi hawa waachwe waendelee kusoma Quran. Pia, wahakikishe na elimu dunia wanafanya vizuri kwenye masomo yao. Elimu zote hizi ni muhimu kwa sababu hata Mtume (Muhammad-S.A.W) aliagizwa asome,” alisema Sheikh Dahiya.

Hata hivyo, Muragili aliagiza kuanzia sasa wanafunzi wasome hadi saa 10:00 jioni si vinginevyo na atakayekaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Wakati huohuo, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha alisema katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kitaifa, halmashauri hiyo imeshika nafasi ya tatu kimkoa na kitaifa ya 82.