Dk Kigwagalla aanza kuhamasisha watu maarufu kupanda Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewaomba watu wa makundi mbalimbali kuungana na yeye Septemba 2019 kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kupitia kampeni ya ‘Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019.’

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla ameanza kuhamasisha makundi mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wasanii ili kuitikia kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro Septemba mwaka 2019.

Lengo la kampeni hiyo ni kuchangisha fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.

Katika   akaunti yake ya Twitter, Waziri Kigwangalla amewaomba baadhi ya wabunge, Nape Nnauye (Mtama-CCM), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), Halima Mdee (Kawe-Chadema) kukubali kuunga mkono kampeni hiyo ya kupanda mlima.

“Nawaalika waandishi wa habari, akina @SalimKikeke1, @venusnyota na wengine; wanamichezo akina @Samagoal77_@EmmanuelOkwi, viongozi akina @jokateM, @kherijames na wengine kushindania nafasi za kupanda Mlima Mrefu kuliko yote barani Afrika, #Kilimanjaro, mwezi septemba 2019,” ameandika Waziri Kigwangalla

Waziri huyo ameandika tena, “Natoa challenge kwa watu mashuhuri ndani na nje ya nchi yetu kuambatana na mimi kwenye Kampeni ya Kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha pesa kwa ajili ya mfuko wa VVU/UKIMWI. Wanasiasa akina @JMakamba@zittokabwe n.k, wasanii akina @OfficialAliKiba@diamondplatnumz@MwanaFA.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Kigwangalla alizindua shughuli ya upandaji Mlima Kilimanjaro lililoshirikisha zaidi ya watu 80 kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kupitia kampeni ya ‘Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019’.

Waziri Kigwangalla alisema mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi si ya Serikali pakee bali ni jamii nzima ikishirikishwa ipasavyo inaweza kuhamasika kukabiliana nao ipasavyo.

Kampeni hiyo ambayo iliratibiwa na Mgodi wa dhahabu ya Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kudhibiti Ukimwi nchi (TACAIDS)  pia imelenga kutunisha mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).

“Takwimu za maambukizi mapya hususan katika kundi la vijana yanatisha na zinahitajika jitihada za makusudi kutoka Katika kundi hilo kudhibiti ugonjwa huo ambao unamaliza nguvu kazi ya Taifa."

“Lazima sisi Kama vijana  tuwe msitari wa mbele kupambana na hali hii, kwa mwaka nimepanga kupanda Mlima huu (Kilimanjaro) na watu mashuhuri ikiwemo wanasiasa na wasanii ili kuchangisha fedha kwaajili ya kudhibiti ugonjwa huu na najua tutafanikiwa," alisema Dk Kugwangalla

Waziri huyo alifurahishwa na kampeni hiyo ambayo miongoni mwa wanufaika ni wapagazi takribani 150 waliopatiwa mafunzo ya kujilinda na VVU na masuala mbalimbali kuhusu udhibiti wa Ukimwi.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa GGM, Richard Jordinson alisema kampeni hiyo imewezesha ukusanyaji wa zaidi ya Sh 13 bilioni tangu ilipoanzishwa miaka 17 iliyopita ambapo taasisi binafsi na mashirika 50 yanayotoa misaada na elimu ya Ukimwi nchini yamenufaika na kampeni hiyo.

Alisema kampeni ya mwaka huu zaidi ya watu 80 wameshiriki ambapo kati yao 32 watapanda mlima, 28 watauzunguka kwa kutumia baiskeli na watu 17 kutoka nchi mbalimbali wameshiriki kampeni hiyo ya kupanda mlima Kilimanjaro.

Awali, Mkurugenzi wa Tacaids, Dk Leonard Maboko alisema kila siku watu zaidi ya 200 huambukizwa VVU ambapo Kati yao asilimia 80 ni vijana kuanzia miaka 15-24 hivyo kampeni hiyo itapunguza maambukizi kwa sehemu kubwa.