Hakuna kifungo jela Sheria ya Takwimu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi akiwasilisha bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Bunge limepitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019, ndani yake ukiwa na marekebisho ya Sheria ya Takwimu (sura ya 351) ambayo yanatoa ruhusa kwa mtu yeyote kutoa takwimu zinazotofautiana na zilizotolewa na Serikali.

Kwa uamuzi huo, kifungu cha 37(4) kinachotoa adhabu kwa mtu anayetoa taarifa za kitakwimu bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kimefutwa.

Kabla ya kufutwa, kifungu hicho kilitoa adhabu kwa makosa hayo ya jinai katika Sheria ya Takwimu ambayo ilikuwa ni jela miezi sita au faini isiyopungua Sh2 milioni au vyote viwili.

Hata hivyo, mtoa takwimu anatakiwa kuzingatia misingi iliyowekwa katika miongozo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Wakati Serikali ikiwasilisha marekebisho hayo, baadhi ya wabunge wakiwamo Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Ally Salehe (Malindi) walisema Serikali imeifanyia marekebisho hayo baada ya kubanwa na nchi wahisani zilizogoma kutoa msaada kutokana na ubaya wa awali wa sheria hiyo.

Sheria ya Takwimu ni miongoni mwa sheria nane zilizokuwa katika muswada huo uliowasilishwa bungeni jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi na kujadiliwa na kupitishwa.

Sheria nyingine zilizofanyiwa marekebisho zilizomo katika muswada huo ni sheria ya makampuni (sura ya 212), sheria ya hakimiliki (sura ya 218), sheria ya filamu na michezo ya kuigiza (sura ya 230), sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali (sura ya 56), sheria ya vyama vya kijamii (Sura ya 337), sheria ya uwakala wa meli (sura ya 415) na sheria ya muunganisho wa wadhamini (sura ya 318).

Katika maelezo yake, Profesa Kilangi alisema pamoja na marekebisho hayo, inapendekezwa kufutwa kwa kifungu cha 37(4) kinachotoa adhabu kwa mtu anayetoa taarifa za kitakwimu bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)

Awali, ilikuwa mchakataji wa taarifa za takwimu alipaswa kuomba kibali kabla ya kusambaza kwa umma, jambo lililozua hali ya sintofahamu.

Makosa kwa mtu yeyote kutoa taarifa zilizopatikana isivyo halali, adhabu yake ilikuwa ni kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua Sh5 milioni au vyote viwili.

“Kama inavyoonekana katika jedwali la marekebisho, inapendekezwa kufutwa vifungu vya 24A na 24B na kuviandaa upya, pia kuongeza vifungu vipya vya 24C, 24D, 24E na 24F kwa lengo la kuweka utaratibu wa kutoa matokeo ya takwimu zinazotofautiana na takwimu rasmi zilizotolewa na Serikali.”

“Marekebisho haya yanapendekeza kuanzisha kamati ya kitaalamu ambayo jukumu lake litakuwa kupokea na kujadili malalamiko yanayotokana na wadau kuhusu usahihi wa takwimu zilizotolewa na umma,” alisema Profesa Kilangi.

Alisema katika sheria hiyo, baadhi ya tafsiri zimefutwa na kuandikwa upya lengo likiwa ni kutoa ufafanuzi wa aina ya taarifa za kitakwimu zinazotokana na sensa, tafiti na takwimu za utawala.

Alisema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaangalia utoaji wa taarifa za kitakwimu ili kuhakikisha zinakidhi na kuzingatia viwango vya miongozo ya kitaifa na kimataifa.

Walishokisema wabunge

Akichangia muswada huo, Ally Salehe alisema huenda marekebisho hayo yamefanyika baada ya Serikali kulisikiliza Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

Alisema mabadiliko ya sheria hiyo yanatenganisha takwimu za utafiti na tathmini, eneo ambalo lilikuwa na utata.

“Kwa sababu takwimu kama sayansi ina vigezo vilevile, unaweza kuvitumia lakini kingine ni namna ya mtu yeyote kuweza kutoa takwimu na NBS watakuwa na haki ya kujibu takwimu hizo,” alisema.

Salehe alisema Serikali imefanya jambo jema kuunda kamati ya ufundi itakayokuwa na jukumu la kutazama kama takwimu zinaenda sawa ama la kwa maana kama zimetimiza masharti ya kisayansi.

Akijadili hoja hiyo, Zitto alisema mabadiliko hayo yamekuja baada ya Benki ya Dunia kuzuia Dola za Marekani bilioni 1.15.

Alitaja sheria alizoziita zisizofaa zikiwamo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Vyama vya Siasa na sheria ya vikokotoo vya pesheni na haki za wafanyakazi akisema, “tulizungumza kuhusu kifungu 24 A na B cha Sheria ya Takwimu kuwa kinaleta matatizo makubwa ya kunyima haki za watu lakini hatukusikilizwa.

“Nina barua ya Wizara ya Fedha kumuomba Rais aruhusu kabla ya mkutano huu wa Bunge Sheria ya Takwimu irekebishwe na mmetii mmeileta imerekebishwa mnawasikiliza zaidi mabeberu kuliko wananchi wenu walioikataa sheria hii,” alisema Zitto.