Hoja mbili za Chadema zawaibua wasomi

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji

Muktasari:

  • Maazimio hayo mawili yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya Chadema na kuungwa mkono na wasomi na wanaharakati ni pamoja na kufungua kesi ya kupinga mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa mara itakaposainiwa na kuandaa rasimu ya muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Dar es Salaam. Maazimio mawili ya Chadema; kufungua kesi ya kupinga mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa mara itakaposainiwa, na kuandaa rasimu ya muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi yameungwa mkono na wasomi, wanasheria na wanaharakati.

Maazimio hayo yalifikiwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni baada ya jitihada za kukwamisha muswada huo bungeni kukwama.

Pia, muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) umekuwa ukipingwa, hasa na vyama vya upinzani kutokana na viongozi wake kuteuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama cha siasa ambacho pia kinashindana, huku wasimamizi wa uchaguzi wakiwa ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia ni wateule.

“Zipo kesi nyingi zilizowahi kutokea ambazo zilipinga miswada iliyokwenda kinyume na katiba, mahakama ni chombo huru hivyo huko ndiyo sehemu sahihi kudai haki hiyo,” alisema John Seka, rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Seka alisema Chadema wakifungua kesi ya kikatiba kueleza namna sheria inavyokwenda kinyume na haki yao kwa mujibu wa Katiba, wanaweza kupata ufumbuzi.

Kuhusu rasimu, Seka alisema kuiandaa ni kitu kingine na kwa sababu ni mawazo yao wanaweza kufanya.

Alisema namna wasimamizi wa uchaguzi wanavyopatikana imewekwa kisheria, lakini haikuzungumza watumike wakurugenzi, bali watumishi wa Serikali hivyo hata walimu wanaweza kusimamia ni utaratibu tu waliojiwekea kuwatumia hao.

Naye mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema msimamo wao ni ule ule kuupinga muswada huo.

Alisema watafanya hivyo mara baada ya kuona nakala ya mwisho ya muswada huo baada ya kujadiliwa bungeni.

“Tutaangalia kama mapendekezo yetu muhimu wameyaweka, kama yametolewa tutapinga mahakamani,” alisema.

“Wanachofikiria kufanya Chadema ni sahihi, sehemu pekee ya kudai haki ya kikatiba ni mahakamani. Hivyo wapo kwenye njia sahihi.”

Kuhusu mpango wa kuandaa rasimu ya NEC, Henga pia alisema Chadema wapo sahihi kama ambavyo wao tayari walishafungua kesi kudai suala hilo.

“Sitazungumzia sana hapa kwa sababu kesi tayari ipo mahakamani tunapinga hilo na jana (juzi) imetajwa, ”alisema Henga.

Mhadhiri mwingine aliyeunga mkono mpango huo ni Profesa Bakari Mohamed wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyesema kupinga sheria mahakamani ni rahisi kwao.

“Matokeo ya kesi hiyo inategemea na majaji wanaoisikiliza, kama ni wapenda maendeleo wataamua kuwa lengo la kuleta utengano. Kama wenye mrengo tofauti wanaweza kusema hawaisikilizi kwa sababu imepitishwa na Bunge na huo ni mhimili unaojitegemea,” alisema.

“Kesi kama hizo zimewahi kutokea mara nyingi kama ile ya kupinga kutokuwapo kwa mgombea binafsi ambayo ni kinyume cha katiba na Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, Marehemu Justice Lugakingira aliamua kuwa ni kweli suala hilo linapingana na Katiba, ingawa hukumu yake ilibadilishwa na Mahakama ya Rufani.”

Kuhusu rasimu ya Tume huru, alisema hatua hiyo itakuwa ni kuonyesha msimamo wao lakini licha ya kuwa na nia njema, bado itategemea watawala kama watakubali kusikiliza.

Alisema kuibua mjadala, kutoa elimu kwa wananchi, kuomba kuungwa mkono na asasi za kiraia ni miongoni mwa mikakati wanayoweza kufanya ili kufikia azma yao.

Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, hatua inayofuata ni Rais John Magufuli kusaini na kutangazwa katika gazeti la Serikali.