Hoja ya uraia pacha inavyowagawa wabunge kiitikadi

Matumaini ya kupata uraia pacha kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi au waliokuwa Watanzania kisha wakaukana uraia wa Tanzania na kuchukua wa nchi nyingine yameendelea kugonga mwamba baada ya Bunge kuliweka kando suala hilo.

Hii si mara ya kwanza, liliibuka pia kwenye Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014 na kuzua mvutano na mwisho wa siku kuwapa Katiba Inayopendekezwa ‘hadhi maalumu na si uraia pacha.

Suala la uraia pacha limekuwa likiibuka kila unapowadia bajeti ya wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa wabunge kuhoji na kutaka uwepo uraia pacha lakini mara zote wamekuwa likikwama.

Alhamisi iliyopita ya Mei 30, wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati ya matumizi kupitisha vifungu vya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Mje ya Sh166.92 bilioni, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ aliibuka tena akiwa amelibeba suala hilo.

Mgawanyiko kiitikadi

Sugu aliibuka na hoja hiyo ambayo ilizua mvutano mkali kwa wabunge wa upinzani kumuunga mkono mbunge huyo huku wale wa CCM wakiungana na Serikali kuipinga.

Inavyoelekea, suala hilo linahusishwa na siasa, maana kila liibukapo wabunge ama hulipinga au kulikubali kwa mtazamo wa kiitikadi. Huenda ni kwa utamaduni wao kupingana kwa kila jambo au ni jambo nyuma ya jambo lenyewe.

Akitoa hoja yake, Sugu anasema umefika muda Serikali ikaanzisha uraia pacha ili iweze kuwasaidia Watanzania wanaoishi ughaibuni ambao wanataka kuwekeza nchi.

Anasema kwa hali ilivyo sasa, Watanzania walioko nje wanapotaka kuwekeza nchi wanahangaika, hivyo kuihoji ‘Serikali inaogopa nini hawa ‘diaspora’ au mnaogopa nini kuwa na urais pacha’ ili kuwawezesha kushiriki kwenye masuala ya uchumi, siasa na mambo mengine kama ilivyo kwa watanzania wengine.

Majibu ya Serikali

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Damas Ndumbaro anasema kwa sasa wameanza kuwatambua Watanzania wanaoishi nje kwa kuwataka kwenda kujiandikisha katika balozi za nchi walipo ili waweze kuwatambua.

“…si suala la kutolea majibu ya harakaharaka, linahitaji mjadala wa pande zote, wabunge wa upinzani, CCM na Serikali,” anasema Dk Ndumbaro.

Sugu hakukubaliana na majibu hayo na kutoa hoja ili wabunge wamuunge mkono na kuichangia. Hoja yake iliungwa mkono na mjadala ukaanza. Wakichangia hoja hiyo, wabunge wa upinzani walimuunga mkono Sugu huku wale wa CCM na Serikali wakiipinga.

Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji anasema, “umefika muda sasa wa Watanzania kupata uraia pacha na hili suala nalifananisha na “joka la mdimu”. Awamu iliyopita, (Jakaya) Kikwete alifanya ziara ughaibuni na kuwaahidi kulishughulikia suala hili.

“Walioko nje wamefanikiwa kiuchumi lakini hawawezi kuja hapa, Waziri wa Ardhi (William Lukuvi) amesikika akisema mtu ambaye si raia hataruhusiwa kumiliki ardhi.

Hivi nchi ambazo wanaotumia uraia pacha zimepata athari gani? Hakuna nchi yoyote duniani kwamba imesabahisha athari na naomba serikali na wabunge tuache roho ya kwa nini,” anasema.

“Joka la mdimu” ni msemo uliotumiwa na aliyewahi kuwa mbunge wa Mchinga, Mudhihiri Mudhihiri bungeni akizungumzia kiongozi mmoja aliyedai alikuwa anakataa kiwanda cha mbolea kujengwa Lindi, akisema huyo kigogo anakikatalia wakati yeye hatafaidika nacho,

kama nyoka wa ndimu anavyozuia ndimu zisiliwe wakati yeye hali ndimu.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda anaungana na Sugu akisema, “Tulikuwa katika nchi ya kijamaa na sasa hatujitambui tuko katika nchi gani na kama alivyosema Khatibu, muhimu ni watoto wetu, ndugu na jamaa kuja nyumbani kuwekeza.”

“Uchumi walionao kule wakija kuwekeza hapa ni faida yetu wenyewe, unapokuwa umeoa au kuolewa kuna milolongo mirefu sana kurudi nyumbani. Tuwape nafasi warejee na wana haki ya kupiga kura, kuwachagua viongozi wanaowataka. Watanzania na wabunge wa CCM muunge mkono,” anasema Mwakagenda

Kana kwamba wito wa Mwakagenda haukusikika, Mbunge wa Namtumbo (CCM), Edwin Ngonyani akanyanyuka na wazo tofauti.

“Suala hili limenigusa, na ndugu zangu tusichanganye. Hatuongelei diaspora 9watanzania waishio nje ya nchi) tunaongelea Watanzania walioukana uraia wa Tanzania na kuwa raia wa nchi zingine.”

“Diaspora bado ni Watanzania wakiwa kule, lakini utaratibu uendelee kusukwa na mchango wao uendelee na wakirudi Tanzania wataendelea kuwa Watanzania. Kama tunaongelea Mtanzania aliyeukana Utanzania, huyu ni msaliti,” anasema Ngonyani.

Ngonyani anaungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Suzan Kolimba anayesema, “Katiba hairuhusu suala hili na hata tukiangalia mfumo wa kujadili na hata Bunge la Katiba hawakufikia mwafaka wa kutoa uraia pacha.

Hao wapewe hadhi maalumu, wapewe upendeleo na kuwekeza. Hao walioukana uraia na kupewa wa nchi nyingine.

Majibu ya mawaziri

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola anasema, “diaspora na Sugu hawana tofauti yoyote, wote ni Watanzania na wana sifa ya kuomba kura lakini tofauti ni Sugu anaishi Mwanjelwa na huyu anaishi nje (ya nchi).”

“Uraia pacha ni ‘ishu’ ya kiusalama, haiwezi kuzungumzwa kwa presha anayoitaka Sugu, kuwa na mahusiano na watu wengine au hao diaspora kwa sababu wanataka tu kuwekeza,” alisema Lugola.

Waziri huyo anasema, “Uwekezaji uko wazi na raia wa nchi nyingine akiona mazingira ya kuwekeza, mimi kama waziri wa mambo ya ndani kwa niaba ya Rais aombe uraia na mimi nitampa.”

Waziri wa Ardhi, Lukuvi anasema diaspora wana haki zote, anaweza kumiliki ardhi na kupewa hati miliki na kupewa makazi lakini mtu ambaye ni mgeni anaweza kupewa kibali maalumu cha uwekezaji na si hatimiliki.

Baada ya mjadala huo, Sugu anahitimisha kwa kusema, michango ya wengi humu (bungeni) inaonyesha kuna suala la fursa na ndio maana nilimwonya na kumwambia Waziri Lugola si wizara ya kutumia maguvumaguvu.

“Huwezi kuhitaji uraia pacha kama uko Mwanjelwa, tunahitaji uraia pacha na leo tupige kura tujue nani anawatakia mema Watanzania wenzetu na tunapata hasara. Wameukana uraia, hawajaukana kwa hiari, wanaukana kwa sababu ndiyo matakwa ya sheria.

Ametoka hapa amesoma, ameelimishwa vizuri, nchi zingine wakimwona ana uwezo na mshahara mnono anaamua kuukana.

Hata hivyo, Bunge halikupiga kura baada ya Naibu Spika Dk Tulia Ackson kusema haiwezekani kupigwa kura kwani mtoaji wa hoja (Sugu) hakuacha muda ili Bunge liamue.