VIDEO: Je unajua ni kitu gani kinachoweza kumvutia Mungu katika maisha yako?

Bwana Yesu apewe sifa, jina langu naitwa Mchungaji Ridhard Godwin kutoka kanisa la Jehoma Mercy lililopo Swaswa jijini Dodoma.

Ni Jumapili njema Mungu ametupatia na ninayo furaha kushiriki nawe neno la Mungu na nikualike usome hakika utajifunza jambo.

Ujumbe nilio nao leo unatoka katika kitabu cha Yohana 1:43 ukiwa na kichwa cha habari kinachosema ‘Ni kitu gani kinaweza kumvutia Mungu kwenye maisha yako?

Amini kwamba kipo kitu katika maisha yako ukikifanya kinaweza kumvutia Mungu.

Katika mstari huu Biblia inaandika, ‘Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akakutana na Filipo, akamwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji ambapo Andrea na Petro walikuwa wanaishi. Filipo naye akamtafuta Nathanaeli akamwambia, “Tumekutana na Yesu wa Nazareti mwana wa Yusufu, ambaye Musa katika Torati na pia Manabii waliandika habari zake.” Nathanaeli akajibu, “Je, inawezekana kitu chochote chema kikatoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo ukajionee mwenyewe.” Katika mistari niliyosoma tunaona wakati Yesu alipokuwa duniani alifanya mambo mengi akikutana na kuwaponya watu wengi.

Kati ya watu hao aliowaponya au kukutana nao kuna wengine aliwaambia ‘njooni mnifuate’ lakini wengine hakuwaambia ‘njooni mnifuate’.

Katika kitabu hicho cha Yohana tunajifunza kwamba siku ya pili Yesu alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo na alipomuona Yesu akamwambia ‘Nifuate’.

Huu ni mfano mmoja wapo tu wa Yesu kumwambia mtu nifuate. Hii ina maana kwamba kuna kitu kimemvutia na kina faida ndani ya mtu huyo ndio maana ameamua kumwambia ‘nifuate’

Katika hali ya kawaida kipo kitu Mungu anavutiwa nacho toka kwako. Tujiulize tu, Je katika kanisa la sasa kuna Wakristo kama wale wa zamani ambao wanaweza kumvutia Mungu?

Ukweli ni kwamba unaweza kuwa Mkristo lakini ukashindwa kumvutia Mungu kwa sababu huna kitu ulichobeba ndani yako. Kitu kinachoweza kumvutia Mungu ni wewe kuwa msaada kwa wengine na hata katika ufalme wake.

Usipokuwa msaada kwa wengine wanaokuhitaji na katika ufalme wa Mungu huwezi kuambiwa ‘nifuate’ kwa sababu hujabeba kitu kinachoweza kumvutia Mungu.

Tusome kitabu cha Matendo 9:36-39 Biblia inasema ‘Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa’

‘ Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, usikawie kuja kwetu.

Ukiangalia hapa utaona anazungumziwa mwanamke mwenye hekima ya ki Mungu na aliyejawa matendo mema na mwenye kusaidia watu wengine.

Mwanamke huyo alikuwa anategemewa na Mungu kwa sababu alitoa msaada kwa wengine waliohitaji msaada huo.

Msaada aliokuwa anautoa ulimfanya afufuliwe kwenye kifo chake, je wewe unafanya nini kwenye nyumba ya Mungu?

Ni kitu gani kinachokufanya uwe na faida nyumbani mwa Mungu ili avutiwe kwako.

Wakristo wengi wanazo huduma ndani yao lakini hawana mpango na huduma hizo hata wamekaa tu nyumbani kwa kuwa hawataki kumtumikia Mungu.

Msomaji wa Mwananchi unapaswa kujua kwamba tunapoishi duniani tujue yapo mambo ambayo tukifanya tunaweza kuwa karibu na Mungu lakini kubwa lazima kuishi katika utakatifu yaani, kuacha uovu na kutenda matendo mema.

Lakini kwa nafasi yako ukisoma Biblia katika kitabu cha Marko 5.18-19 utakutana na ujumbe unaoonyesha kuwa Yesu akaenda kwa mgonjwa mwenye mapepo lakini roho ya kuhubiri ikawa ndani yake.

Kwa hiyo Yesu alipoenda kwa huyo mtu akamponya na kumtuma aende kuhubiri wa kwao. Kwa hiyo kitu kilichomvutia Yesu kwa huyo mtu ni ile roho ya kuhubiri iliyokuwa ndani yake.

Yesu aliona haina haja tufuatane kwa sababu ndani yako kuna nguvu ya kuhubiri na watu wakaelewa mambo ya ajabu ambayo Mungu amekutendea.

Kwa hiyo kuna wakati mtu unaweza kuwa na huduma ndani yako lakini umefungwa lakini ukifunguliwa utamvutia Mungu kwa sababu utaanza kumtumikia Mungu.

Unaweza kuwa na pepo la umaskini, magonjwa na wakati mwingine kukata tamaa kabisa ukidhani hakuna jambo lolote ndani yako linaloweza kuwa kituvutio kwa Mungu, hapana.

Unachohitaji kwenye maisha yako ni kufunguliwa. Jitahidi kuwa karibu na Mungu kwa kuhudhuria ibada na kukutana na watumishi wa Mungu wakusaidie ili kile kilicho ndani yako kifunguliwe nawe uanze kumtumikia Mungu na kuwa kivutio kwake.

Amen.

Mahubiri haya yameandaliwa na Tumaini Msowoya