Kamati ya Bunge yashauri mambo 11 wizara ya ulinzi

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Victor Mwambalaswa akisoma maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeshauri mambo 11 ikiwamo kutoa fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya utunzaji wa zana, magari na mitambo katika mwaka wa fedha 2018/19.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeshauri mambo 11, ikiwamo kutoa fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya utunzaji wa zana, magari na mitambo ya kijeshi katika mwaka wa fedha 2018/19.

Mjumbe wa kamati hiyo, Victor Mwambalaswa ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 16 wakati wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2019/2020.

“Kamati inatambua juhudi kubwa za Serikali katika kugharamia kwanza maeneo ya kimkakati na miradi michache mikubwa. Hata hivyo kamati inaendelea kushauri kuwa upo umuhimu kwa wizara hii kuongezewa ukomo wa bajeti kulingana na mahitaji yake halisi,” amesema.

Amesema wanaitaka Serikali ione umuhimu wa kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni ya kimkataba kwa kutenga fedha zaidi ya miradi ya maendeleo kwa wizara hiyo.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19, kati ya Sh112 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh105bilioni sawa na asilimia 93 ya fedha zilizotolewa zilitumika katika kulipa madeni ya kimkataba.

“Kulipa madeni hayo kwa wakati kutaisaidia Serikali kuokoa fedha zinazoongezeka kwa ajili ya malipo ya riba, vilevile kuelekeza fedha nyingine katika maeneo mengine ya maendeleo,” amesema.

Mwambalaswa amesema wanaitaka Serikali itoe fedha zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kufanya tathmini na kulipa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na jeshi.

Amesema hadi kufikia Machi mwaka huu, asilimia 14.32 tu ya fedha zilizoidhinishwa ndiyo zimetolewa.

Pia wameshauri Serikali kutoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha makazi ya wanajeshi chini ya fungu 57 ambalo ni wizara.

Amesema hadi Machi mwaka huu Sh 208.26 milioni sawa na asilimia 1.47 tu ya fedha zilizotengwa ndiyo zimetolewa.