Kauli ya Dk Bashiru kutaka polisi kutotumia nguvu yagusa kila kona

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally

Dar es Salaam. Wasomi na wanasiasa nchini wameunga mkono kauli ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyelitaka Jeshi la Polisi kutotumia nguvu kushughulikia migogoro ya kisiasa huku, mwenzake wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akisema kauli hiyo imechelewa kutolewa.

“Polisi badala ya kutoa huduma wamekuwa wakiwanyanyasa watu, malalamiko yamekuwa yakitolewa na wananchi wote hasa watu kutekwa, viongozi wa dini wanasumbuliwa, wapinzani wananyanyaswa,” alisema Dk Mashinji na kuongeza kwamba hiyo italeta mabadiliko endapo Dk Bashiru ataamua kwa dhati kushirikiana na wadau wengine kusimamia utekelezaji wake.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo juzi katika mji mdogo wa Kibaya wilayani Kiteto, Manyara akisema hakuna ulazima wa polisi kutumia mabavu wakati wa kutatua migogoro.

Alisema nguvu ya ziada inapaswa kuanza kutumika endapo itaonekana kuwa bila mabavu, mambo hayawezi kuwa sawa hadi lifanyike jambo hilo.

“Kwa kadri tutakavyoona vyombo vyetu vya ulinzi na usalama havitumii mabavu ndivyo tukakavyojipima kwamba mfumo wetu wa kisiasa na uongozi na demokrasia unafanya kazi vizuri,” alisema Dk Bashiru,

Katika maelezo yake ya jana, Dk Mashinji alisema malalamiko dhidi ya polisi yamekuwa yakitolewa na watu wengi na inaonekana kuwa tatizo sugu, “ndio maana nasema kauli ya Dk Bashiru imekuja kwa kuchelewa ila tukishirikiana kwa pamoja na kuhakikisha inasimamiwa, inaweza kubadilisha yanayoendelea.”

Wakati Dk Mashinji akisema hayo, mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kauli hiyo imekuja kwa wakati ila kitu muhimu kinachotakiwa kufanyika ni kusimamia ili itekelezwe kwa vitendo.

Alisema hakuna sababu ya kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama katika kuendesha masuala ya kijamii badala ya kutumia mfumo wa kiraia.

“Nchi zote zilizoingia kwenye machafuko ukifuatilia utaona mambo yalianza kama hivi vyombo vya dola kutumika kuwakandamiza wananchi. Sisi hatujafikia hatua ya kila kitu kusimamiwa na jeshi au polisi.

“Kauli ya Dk Bashiru inapaswa kupongezwa na sasa tuone ikitekelezwa kwa vitendo isiwe tu yanazungumza halafu utekelezaji wake haupo, polisi sasa wamekuwa wakivamia mikutano hata vikao vya wanaharakati, hii si sawa,” alisema Olengurumwa.

Tangu Dk Bashiru alipotoa kauli hiyo, kumekuwa na mjadala mzito hadi mtandaoni, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliweka kwenye ukurasa wake wa Twitter, habari iliyotolewa na tovuti ya Mwananchi kuhusu kauli hiyo na kuandika ujumbe uliosemeka “Huyu ndio Dk Bashiru Ally ninayemjua”.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alipongeza kauli hiyo na kueleza kuwa Dk Bashiru ni mtu ambaye anajaribu kutetea demokrasia.

Alisema kauli hiyo kutolewa na katibu mkuu wa chama tawala inaleta matumaini kuwa huenda siku za usoni kukawa na mabadiko yanayolenga kuhakikisha demokrasia na utawala bora vinachukua nafasi yake.

“Ninavyomuona anajitahidi kupambana na mambo yanayolenga kukandamiza demokrasia. Ingawa ameshindwa kuwa muwazi katika nyanja gani polisi wasitumie nguvu, ukifuatilia kwa kiasi kikubwa polisi wanatumia nguvu kupambana na wapinzani,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga alisema polisi wanatakiwa kulinda usalama wa raia na sio kuwakosesha raha hivyo alichokisema Dk Bashiru ndicho kinachotakiwa kufanyika.