Kisena, mkewe walivyoachiwa huru kisha kushtakiwa upya

Thursday May 16 2019

Mkurugenzi wa Mradi wa mabasi yaendayo haraka

Mkurugenzi wa Mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena (wa pili kulia) na mkewe Florencia Membe (kushoto) wakirejeshwa mahabusu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena, mkewe Florencia Membe (43) na wenzao watatu wameunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi namba 38 ya 2019, wakikabiliwa na mashtaka 19 likiwamo la kuisababisha Udart hasara ya Sh2.4 bilioni.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni pamoja na Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Chen Shi (32).

Washtakiwa hao waliunganishwa katika kesi hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile na wakili wa Serikali Gloria Mwenda muda mfupi baada ya kufutiwa kesi mbili tofauti zilizokuwa zikiwakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba na Hakimu Rwizile.

Mashtaka dhidi yao yalifutwa baada ya upande wa mashtaka kuomba hivyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo 2002 kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi hizo na Mahakama kuridhia na kuwaachia huru.

Hata hivyo, washtakiwa hao waliendelea kushikiliwa na baadaye waliunganishwa na kusomewa kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi ambapo wanakabiliwa na mashtaka 19 yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali cha Ewura, kuuza mafuta kwenye makazi yasiyoruhusiwa eneo la maegesho ya magari.

Pia wanakabiliwa na mashtaka manne ya utakatishaji fedha, manne ya kutoa nyaraka za uongo, manne ya kughushi, mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara.

Wakili wa Serikali, Mwenda akiwasomea mashata hayo mapya jana, alidai walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 2012 mpaka Mei 31 mwaka jana.

Wanadaiwa kati ya Januari Mosi 2011 na Mei 31 mwaka jana katika maeneo tofauti wakiwa na watu wengine, waliratibu shughuli za kihalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Pia inadaiwa kati ya Januari Mosi 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani washtakiwa Robert, Kulwa na Florencia akiwa mkurugenzi wa kampuni ya Zenon Oil Gas Limited alijenga kituo cha mafuta kinachoitwa Zenon Oil and Gas katika karakana ya kampuni ya Udart bila ya kuwa na kibali kutoka Ewura. Na kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2015 wakiwa Dar es Salaam waliiba Sh1.2 bilioni mali ya kampuni ya Udart.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ambayo iliahirishwa hadi Mei 28.

Advertisement