Klabu Mekus yashinda kesi mahakamani

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,

Moshi. Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi limeagiza biashara ya kituo cha mafuta na klabu maarufu ya Mekus Bristol, iendelee kawaida na kampuni ya Oryx Oil Ltd itoe mkataba wa miaka miwili.

Hayo yamo katika uamuzi wa mwenyekiti wa baraza hilo alioutoa Mei 15, katika maombi yaliyowasilishwa na kampuni ya Community Petroleum Ltd inayoendesha biashara hizo.

Kampuni hiyo iliwasilisha maombi hayo dhidi ya kampuni ya Oryx na Alphonce Mwacha, ikitaka Baraza hilo likazie hukumu iliyotokana na shauri namba 157/2017 lililosuluhishwa nje ya Mahakama.

Katika makubaliano hayo, Oryx na Mwacha walikubaliana kuipa mkataba wa miaka miwili, Community Petroleum Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Peter Kaale.

Hata hivyo, licha ya uwapo wa makubaliano hayo, Oryx na Mwacha hawakutekeleza na kuitoa kwa nguvu kampuni ya Community na kubomoa mgahawa wa Mekus.

Katika uamuzi wake, mwenyekiti wa Baraza hilo, James Silas, alionyesha kusikitishwa na kitendo cha Oryx na mshirika wake kumuondoa kwa nguvu Community licha ya uwapo wa zuio la Mahakama.

Hivyo, aliiagiza Oryx kuandaa mkataba wa miaka miwili wa kuipatia Community eneo hilo kama walivyokubaliana. Pia, ametoa amri ya kurejeshwa kwa Community kuendesha kituo hicho na mgahawa wa Mekus Bristol mtu yeyote haruhusiwi kuibughudhi au kuingilia biashara zake. Hata hivyo, Kaale kupitia video inayosambaa mitandaoni tangu juzi, amelalamika kuwa licha ya hukumu hiyo hawajaruhusiwa kuendelea na biashara na hapati ushirikiano wa Polisi waliopaswa kusimamia utekelezaji uamuzi wa Baraza.

Naye kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah alisema kama Kaale anaamini ana mkataba wa upangishaji sheria itumike.