Kuadimika kondomu kwatishia Ukimwi kuongezeka

Muktasari:

Upungufu wa mipira ya kinga maarufu ‘kondomu’ umetajwa kujitokeza nchini ikiwemo Njombe na Shinyanga ingawa Serikali imedai kuwa upungufu huo unatokana na kubadili mfumo wa usambazaji.

Dar es Salaam. Wakati wadau wakihofia kuadimika kwa mipira ya kiume, maarufu kwa jina la kondomu kwamba kunaweza kusababisha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Serikali imesema tatizo hilo linatokana na kubadili mfumo wa usambazaji.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema licha ya Serikali kusambaza mipira hiyo, walikuwapo wasambazaji binafsi ambao kwa sasa wameachia jukumu hilo kwa Wizara ya Afya.

Dk Ndugulile alisema kwa sasa wizara itakuwa ikisimamia ununuzi na usambazaji, hivyo utaratibu ambao ulikuwapo kwa taasisi kupewa fedha za kusambaza bidhaa hizo kwa bei nafuu, umebadilika.

“Serikali itakuwa inanunua na kugawa bure katika maeneo yote yanayohusika kwa jamii, hivyo tumelibaini hilo tatizo na kwa hiki kipindi cha mpito tumehakikisha tunapata kondomu za kutosha na zitapatikana kabla ya mwisho wa mwezi huu,” alisema.

Kondomu zilizoadimika ni zile zilizokuwa zikitolewa bure au kwa bei nafuu kwa watu mbalimbali, kama taasisi za elimu na maeneo yenye maambukizi makubwa.

Wakati Serikali ikiahidi kumaliza tatizo hilo mapema, taasisi zisizo za kiserikali zinasema lisatasababisha ongezeko la maambukizi, hasa katika mikoa iliyoathirika zaidi kama Njombe.

“Sikika tunafuatilia suala hili. Kwa ujumla wanaotakiwa kuhakikisha uwepo wa kondomu, wahakikishe zipo muda wote sababu kuna mifumo ambayo ikitumika sawasawa huduma zote za afya zinazotakiwa kuwapo, zitaifikia jamii kwa wakati,” alisema mkurugenzi mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria.

“Kuna mahali katika huu mfumo kuna kuna uzembe au vinginevyo, lakini madhara yake maambukizi yanaweza yakatokea kama hakutakuwepo na kinga.”

Lakini mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema hawana taarifa za kuadimika kwa kinga hiyo.

“Wanaoshughulikia suala hilo kwa sasa ni kitengo cha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa cha Wizara ya Afya. Nao wananunua MSD na waganga wakuu ndiyo wanaotakiwa kuhakikisha zinafika katika maeneo husika,,” alisema Dk Maboko.

Kondomu zauzwa hadi Sh12,500

Upungufu huo umekuwa fursa kwa wakazi wa mji wa Makambako, moja ya maeneo yenye tatizo kubwa la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mganga mkuu wa mji wa Makambako, Dk Ernest Kingu alisema baada ya kusitishwa kwa huduma kutoka PSI, kinga zilizokuwa zinauzwa Sh5,000 kwa pakiti sasa zinapatikana kwa Sh12,500.

Alisema kila walipopata kinga hizo kutoka MSD au PSI walisambaza sehemu zote muhimu kama hotelini na kwenye baa.

Alisema sehemu ambazo Serikali ilikuwa inasambaza, kondomu bado zipo lakini tatizo ni maeneo yaliyokuwa yanahudumiwa na taasisi nyingine.