Kwa nini figo hushindwa kufanya kazi?

Figo kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama kidney au Renal. Pia ni ogani muhimu ya ndani ya tumbo yenye umbile mfano wa maharagwe.

Katika mwili usio na dosari yoyote tuna figo mbili; upande wa kushoto na kulia ambazo ndizo zinazotuwezesha kuchuja damu na kutoa taka mwili zinazotolewa kwa njia ya mkojo.

Magonjwa sugu mawili ndiyo chanzo cha ugonjwa sugu wa figo, magonjwa hayo ni kisukari na shinikizo la damu.

Magonjwa haya yasiyoambukiza ndiyo yanayochangia idadi kubwa ya wagonjwa wa figo kuongezeka.

Hali hiyo pia husababisha wagonjwa hawa kuwa na tatizo la kudumu la figo kushindwa kufanya kazi au kwa neno jingine tunaita ugonjwa sugu wa figo.

Matatizo mengine ya kiafya yanayochangia ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na kuharibika kwa mishipa ya damu katika figo tatizo linalojulikana kitabibu kama Atheroscreosis hivyo kusababisha figo kupata damu kidogo.

Sababu nyingine uwepo uvimbe wenye maji ndani katika figo(cyst), magonjwa ya kurithi ya figo ujulikana nao kama Pollycystic kidney disease, ugonjwa ujulikanao kama Sytemic lupus erythematus

Vile vile utumiaji wa baadhi ya dawa za antibiotiki kiholela au katika kiwango cha dozi kubwa cha baadhi ya antibiotiki na dawa za maumivu kwa muda mrefu ikiwamo Ibobrufen na Acetaminophen (paracetamol).

Magonjwa mengine ni pamoja na hitilafu ya kinga ya mwili kushambulia tishu za figo, uwapo wa vitu vinavyoziba mishipa midogo ya figo ikiwamo mawe, maambukizi ya bakteria katika figo, saratani na uvimbe katika figo.

Pia, dawa za matibabu ya fangasi ikiwamo utumiaji wa dawa ya Fluconazole pasipo tahadhari au kiholela. Ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Uthibiti wa Magonjwa cha nchini Marekani (CDC), ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayojitokeza na kuchukua chati za juu nchini humo.

Ni vizuri kuchukua tahadhari mapema kwa kuepuka vihatarishi vya kupata shinikizo la damu na kisukari kwani madhara yake ndiyo chanzo kikubwa cha ugonjwa sugu wa figo. Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu=