Kwa wanaoogopa kupima, hizi zinaweza kuwa dalili za UKIMWI

Watu wengi wamekuwa waoga kupima virusi vya Ukimwi kutokana na madhara ya kisaikolojia yanayojitokeza baada ya mtu kujijua ana ugonjwa huu, hivyo wengi huamua kubaki na sintofahamu tu. Kwa ambao hawajawa tayari kupima Ukimwi, dalili zifuatazo zinaweza kuwa za ugonjwa wa Ukimwi.

Maumivu ya koo na kichwa yanayodumu. Ni kawaida sana kupata maumivu ya kichwa na koo yanayodumu ambayo mara nyingi yanasababishwa na magonjwa ya muda mfupi kama malaria na mengineyo, maumivu ya koo na kichwa mara tu baada ya kupona magonjwa hayo ya muda mfupi.

Pia maumivu ya koo na kichwa yanayodumu muda mrefu yanaweza kuwa ishara ya maambukizi ya Ukimwi, mathalani yakidumu muda mrefu kwa mtu ambaye hajapima virusi vya Ukimwi na hajajua kama ameshaambukizwa au la. Mbaya zaidi ikitokea mtu anayepata dalili hizi awe amewahi kufanya ngono bila kinga na idadi kadhaa ya watu kwa miezi ya karibuni.

Afya ya ngozi kubadilika. Miezi michache baada maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kuna baadhi ya ishara zinaweza kujionyesha kwenye ngozi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, virusi vya Ukimwi vinaenda kupambana na mfumo wa kinga mwilini, mfumo huo ukizidiwa nguvu na virusi ndipo Ukimwi unapoanza kuathiri afya ya mwili mzima ikiwemo afya ya ngozi.

Baada ya mfumo wa kinga za mwili kushuka ni rahisi kwa ngozi kupata baadhi ya magonjwa ya ngozi ikiwemo chunusi sugu, ngozi kubadilika rangi na kuwa na mabaka mabaka.

Japo si kwa wote hutokea dalili hii lakini ni vigumu pia kutofautisha ni sababu ipi inayosababisha matatizo haya ya ngozi, lakini kama yakidumu muda mrefu ni vyema kupata vipimo stahiki.

Kichefuchefu, kuharisha na kutapika. Ni kawaida sana mtu kupatwa na hali hizi mathalani inapotokea mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula umevurugika kutokana na kula au kunywa vitu visivyo salama kwa afya.

Lakini hali hizi ni dalili za muda mfupi tu hutoweka baada ya kupatiwa msaada wa kiafya. Lakini ifahamike kuwa, kwa zaidi ya asilimia 50 ya watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi hukumbwa na hali hizi hasa wakati ambao tayari virusi hivi vimeshatengeneza ugonjwa wenyewe wa Ukimwi.

Mabadiliko yanayojitokeza kwenye kucha. Dalili nyingine inayojitokeza baada ya kupata maambukizi ya ya Ukimwi ni mabadiliko yanayojitokeza kwenye kucha.

Kwa tafsiri nyingine ni kwamba mabadiliko yanayojitokeza kwenye kucha mara zote yanaongea kitu kuhusu mwenendo afya ya mtu husika na hasa inapofikia kwenye virusi vya Ukimwi.

Huenda hukulijua hili msomaji. Mara nyingi kwa mtu mwenye virusi vya Ukimwi huonyesha dalili mbali mbali kwenye kucha zake kama vile kucha kuonekana zimekauka, kubadilika rangi, na hata kumeguka.

Hii hutokana na maambukizi ya fangasi yanayoshambulia kucha ambayo huwa yanatokana na kudhoofika kwa mfumo wa kinga mwilini kulikosababishwa na virusi vya Ukimwi.