VIDEO: Maalim Seif kukaribishwa rasmi Zanzibar, mamia wamiminika kumsikiliza

Muktasari:

  • Unaweza kusema Maalim Seif Sharif Hamad leo anakaribishwa rasmi katika ofisi za ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar, tayari mamia ya wananchi wameanza kumiminika katika viwanja vya Vuga kwa ajili ya kumshuhudia na kumsikiliza

Unguja. Viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo wameanza kuwasili katika viwanja vya Vuga mjini Unguja kushiriki mkutano wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Machi 18, 2019 Maalim Seif alijiunga na ACT-Wazalendo na leo Alhamisi Machi 21, 2019, mwanachama huyo mpya anakaribishwa rasmi katika ofisi za chama hicho visiwani Zanzibar sambamba na kutoa neno kwa wananchi na viongozi wa chama chake hicho kipya.

Mwananchi lililopo katika viwanja hivyo limeshuhudia wananchi hao wakiwa wamevalia sare za chama hicho huku wakisubiri kumshuhudia na kumsikiliza Maalim Seif.

Ratiba iliyotolewa na chama hicho inaeleza kuwa mbali na mambo mengine, lengo kuu ni kumkaribisha Maalim Seif kwenye ofisi za ACT Zanzibar.

Kaimu Katibu Uenezi wa ACT Zanzibar Seif Hamad Suleiman, amesema kufanyika kwa mkutano huo hakuna maana ya kuanza mikutano ya hadhara bali ni kuwakaribisha wanachama wapya.

“Lengo si kuanza mikutano bali kuwakaribisha wageni ndani ya chama chetu,” amesema Suleiman.