MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Maelezo ya ungamo yaibua mabishano makali

Moshi. Maelezo yanayodaiwa kuwa ni ya ungamo la mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastica, jana yaliibua mabishano makali ya kisheria.

Mabishano hayo yaliibuka wakati shahidi wa 14 wa upande wa mashitaka, Irene Mushi, ambaye ni mlinzi wa amani, alipoiomba Mahakama Kuu ipokee maelezo hayo kama kielelezo cha kesi hiyo.

Jopo la mawakili wa utetezi linaloundwa na Elikunda kipoko, David Shillatu, Wakisa Sambo na Patrik Paul, lilipinga kupokelewa kwa maelezo hayo.

Akitoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande, shahidi huyo alieleza kuwa Novemba 20,2017, alijulishwa na bosi wake kuhusu kuletwa kwa mshitakiwa huyo.

Irene, ambaye pia ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Moshi mjini, alimueleza Jaji Frimin Matogolo kuwa kabla ya kuchukua maelezo hayo, alimueleza haki zake.

“Nilimuuliza kama ameshurutishwa kuja kutoa maelezo yake, akasema hapana. Amekuja kutoa mwenyewe na pia nilimuuliza kama yuko free (huru) kunieleza akasema yuko free,” alisema.

“Nilimuuliza pia kama anajua maelezo hayo yanaweza kutumika kama sehemu ya ushahidi, akasema ‘ndio’. Kila nilichokuwa namuuliza nilikuwa nakiandika kwenye ile karatasi ya mwongozo,” alisema.

Shahidi huyo alieleza utaratibu aliotumia kuandika maelezo hayo kwamba kila ambacho mshitakiwa alikuwa akimueleza ndicho alichokiandika na mwisho alimsomea na baadaye wote kuweka sahihi zao.

“Hili ni ungamo (la mshitakiwa wa kwanza) ambalo nililiandika mimi na ningependa mahakama ilipokee kama kielelezo (kielelezo namba P7) cha sehemu ya ushahidi wangu,” alisema shahidi huyo.

Hata hivyo, Wakili Kipoko alipinga kupokelewa kwa kielelezo hicho na kueleza sababu mbili kuwa, kina mapungufu ya kisheria na hakikidhi masharti ya hiyari.

Baada ya hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Pande alisema kwa vile upande wa utetezi wamewasilisha pingamizi hilo, ni vyema mahakama ikasikiliza pingamizi hilo kisha kutoa uamuzi.

Jaji alikubaliana na hoja za kuwasilisha kwa hoja za pingamizi na Wakili Shillatu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwasilisha hoja hiyo akisema suala la uchukuaji maelezo ya ungamo ni la kisheria.

Wakili Shillatu alidai uchukuaji wa maelezo ya ungamo (extra judicial statement) ulitolewa Julai 1964 na Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia kijitabu chake cha muongozo kwa mlinzi wa amani.

“Muongozo huo ulianza kufanya kazi tangu Julai 1964 siku ambayo the Magistrate Act (sheria ya Mahakimu) ilianza kufanya kazi na ulikuwa sehemu ya sheria zinazoongoza mahakama zetu,” alieleza.

Wakili Shillatu alieleza kifungu cha 72(3) cha sheria hiyo ya Mahakimu, kinaeleza mambo sita ambayo Hakimu anayechukua maelezo ya ungamo anapaswa kuyazingatia, lakini akasema atataja mawili.

“Moja ni muda na tarehe aliyokamatwa mshitakiwa na pili ni sehemu ambayo mtuhumiwa alilala kabla ya tarehe aliyopelekwa mbele ya mlinzi wa amani,” alieleza Wakili Shillatu.

“Lakini kwenye hii extra judicial statement ambayo wenzetu (upande wa mashitaka) wanaileta hakuna sehemu ambayo inaonyesha muda ambao mtuhumiwa alipelekwa mbele ya mlinzi wa amani,” alisema.

“Number two (namba mbili) ni kwamba mtuhumiwa hakuulizwa na mlinzi wa amani alilala wapi. Hakuna mahali ilipoandikwa (kwenye maelezo) mshitakiwa alilala wapi.”

Wakili Shillatu alisema kwa kuzingatia hoja hizo mbili, maelezo hayo ya ungamo la mshitakiwa huyo wa kwanza yanakosa sifa ya kupokelewa kama kielelezo cha kesi hiyo.

Kwa upande wake, Wakili Sambo aliunga mkono hoja ya Wakili Shillatu lakini akaenda mbali zaidi na kuegemea kifungu cha 50 na 51 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya 2002.

“Chini ya kifungu cha 50 na 51 cha CPA ni matakwa ya kisheria kwamba maelezo yachukuliwe ndani ya saa nne na yasizidi nane baada ya mtuhumiwa kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi,” alieleza.

“Kwa maelezo yake (shahidi), mshitakiwa alikamatwa 17.11.2017 na alipelekwa kwake 20.11.2017 na masaa yaliyotakiwa kisheria yalikuwa yameshapita na hakuna maombi ya kuongeza muda,” alisema.

Mawakili hao, Kipoko na Paul waliunga mkono hoja za mawakili wenzao na kuongeza kwa kuainisha maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufaa yanayombana jaji kuyafuata na kuyatupa maelezo hayo.