Mahakama yakataa hati ya mauzo kiwanja cha Gugai

Aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai

Muktasari:

  • Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kupokea mkataba wa mauzo ya kiwanja uliotolewa na upande wa mashtaka kama kielelezo katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa mhasubu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu

Dar es Salaam. Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kupokea mkataba wa mauzo ya kiwanja uliotolewa na upande wa mashtaka kama kielelezo katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa mhasibu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu.

Mkataba uliokataliwa mahakamani hapo unamuhusu Gugai pekee ambaye mbali na mashtaka hayo, pia anakabiliwa na shtaka la kumiliki mali zilizozidi kipato chake halali.

Mahakama hiyo imekataa kupokea mkataba huo ili utumike kama kielelezo katika kesi hiyo kwa sababu haujakidhi matakwa  ya sheria ya ushahidi.

Akitoa uamuzi huo leo Alhamisi Julai 18, 2019  Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba amesema upande wa utetezi ulipinga mkataba huo usipokelewe mahakamani kama kielelezo kutokana na kukiuka sheria ya ushahidi.

Hakimu Simba amesema baada ya kupitia hoja za pande zote amebaini kuwa mkataba huo haujakidhi matakwa ya sheria ya ushahidi.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya ushahidi ili nyaraka iweze kupokelewa mahakamani inatakiwa iwe halisi na si nakala.

" Nyaraka iliyotolewa na upande wa mashtaka itumike kama kielelezo katika kesi hii, haijakidhi sheria ya ushahidi namba 66 na 68.”

“Kutokana na sababu hii mahakama imekataa kupokea nyaraka kutumika kama kielelezo katika kesi hii," amesema Hakimu Simba.

Baada ya kueleza hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 31, 2019 itakapotajwa na Agosti mosi na Agosti 6, mwaka itakapoendelea na ushahidi.

Julai 11, 2019  wakili wa utetezi, Semi Malimi alipinga nyaraka hiyo iliyotolewa na upande wa mashtaka, isipokelewe mahakamani hapo kwa sababu haikufuata sheria.

Malimi amedai nyaraka yoyote ambayo inatolewa mahakamani lazima iwe halisi na sio kopi.

Amedai kama inatolewa kopi basi yangekuwepo  na mazingira fulani ya kutolewa kwa kopi na pia upande wa mashtaka hawajaeleza chochote kuhusu nyaraka halisi.

Akijbu hoja hizo Wakili wa Serikali mwandamizi, Awamu Mbagw amedai  nyaraka halisi anayo mshtakiwa mwenyewe, kuomba mahakama kupokea kielelezo hicho na hoja za upande wa utetezi zitupiliwe mbali.

Tayari mashahidi 20 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi ni Abubakari  Hamisi, aliyemuuzia Gugai kiwanja eneo la  Ununio .

Hamisi kama mwanafamilia ya Amina Kilemba alikubaliana na familia hiyo kumuuzia  Gugai  kiwanja namba 64 kwa  Sh80 milioni

Shahidi huyo amedai alilipwa na Gugai kiasi hicho cha fedha  lakini  mkataba ambao walisaini ulionyesha malipo ya Sh60 milioni.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake wanakabiliwa na makosa 43, makosa 19 kati ya hayo  ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari mwaka  2005 na Desemba mwaka 2015.

Inadaiwa mshitakiwa  akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni zisizolingana na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Imeandikwa na Hadija Jumanne, Sifras Kingamkono na Daniel Francis