Mahakama yawakataa wadhamini kambi ya Maalim Seif, Lipumba

Muktasari:

  • Leo Jumatatu, Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh kuhusu bodi halali ya Chama cha Wananchi (CUF)

Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) wa kambi ya Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Februari 18, 2019 na Jaji Dk Benhajj Masoud baada ya kubatilisha uteuzi wao.

Vile vile Jaji Masoud amesema majina yaliyokuwa yamependekezwa na kambi ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad hawakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hiyo kwa kuwa nao hakuwa wamekidhi matakwa ya sheria.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu uamuzi huo, mmoja wa mawakili wa CUF  kambi ya Maalim Seif, Juma Nassoro amesema kwa uamuzi huo, wajumbe wa bodi waliokuwepo wanaendelea na majukumu yao licha ya kwamba muda wao umeshaisha hadi hapo wajumbe wengine watakapoteuliwa.

Mbunge wa Malindi (CUF) Ally Saleh alifungua kesi hiyo akipinga uamuzi wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) wa kuwaidhinisha wajumbe waliopendekezwa na kambi ya Profesa Lipumba kuwa wajumbe wapya wa bodi hiyo.