Majibu ya Serikali kuhusu posho za madiwani, wenyeviti wa mitaa

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 15 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imesema kwa sasa haiwezi kupandisha posho za madiwani wataendelea kulipwa kutokana na ukusanyaji mapato ya halmashauri husika

Dodoma: Serikali imesema kigezo kikubwa cha kupandisha posho za madiwani ni uwezo wa halmashauri kukusanya mapato ya ndani.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 24, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara akijibu swali la mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM), Flatei Massay.

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali kuongeza posho na mishahara ya madiwani.

Katika majibu yake, Mwita amesema Serikali itaendelea kuthamini na kutambua kazi nzuri inayotekelezwa na madiwani na kuongeza posho kadri makusanyo ya mapato yanavyoimarika.

Mwita amesema Serikali ilipandisha posho ya madiwani kupitia waraka wa mwaka 2012 kutoka Sh120,000 hadi Sh250,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3.

Amesema katika mwaka wa fedha 2014/15, Serikali ilipandisha tena posho za madiwani kupitia waraka wa mwaka 2014 kutoka Sh250,000 hadi Sh350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40.

“Pia, Serikali inalipa posho ya madaraka kwa wenyeviti wa kamati Sh80,000 kwa mwezi na posho ya kikao Sh40,000 kwa mujibu wa waraka wa 2007,” amesema Mwita.

Katika swali lake la nyongeza, Massay alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kubadili utaratibu wa kuwalipa madiwani hao, akitaka malipo yao yafanywe na Hazina kwa kuwa baadhi ya halmashauri hazina uwezo, huku akihoji ni lini wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji nao wataanza kulipwa.

“Halmashauri ambayo haina uwezo wa kujiendesha inapaswa kufutwa. Katika hili hatujapata malalamiko hizi halmashauri zinawalipa madiwani kupitia mapato yake ya ndani,” amesema Waitara na kuongeza:

“Tumeshaelekeza kila diwani alipwe stahiki zake. Mpango wa kuwalipa wenyeviti wa mitaa kuna maelezo ya Serikali asilimia 20 ya mapato ya halmashauri kulipwa wenyeviti wa mitaa na vitongoji. Kuendelea kuwalipa asilimia nyingine zaidi inategemea uwezo wa Serikali.”

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa naye aliuliza swali la nyongeza akitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kuwalipa mshahara wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutokana na asilimia 20 katika baadhi ya halmashauri kuwa ndogo huku iddi ya viongozi hao ikiwa kubwa.

“Tungeweza kuwalipa mishahara ila ni wengi na wanafanya kazi kubwa tunalitambua hilo. Tumeelekeza walipwe ingawa kiwango ni kidogo lakini kuna maeneo  hawa watu hawalipwi stahiki zao. Uwezo wa Serikali ukiruhusu viongozi wenzetu watalipwa stahiki zao,” amejibu Waitara.