Makalla utabiri umetimia

Thursday May 16 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Dalili za kuvuliwa madaraka ya ukuu wa mkoa kwa Amos Makalla zilianza kuonekana mapema.

Dalili hizo zilianza kuonekana wakati Rais John Magufuli katika mmoja ya mikutano yake aliyoifanya katika ziara zake za kikazi mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hivi karibuni alipogusia utendaji kazi wa kada huyo wa CCM.

Baada ya utabiri huo kutimia juzi usiku, Makalla aliyekuwa mjini Dodoma jana alilazimika kusafiri kilomita zaidi ya 500 hadi Katavi kwenda kukabidhi ofisi.

Makalla, ambaye amewahi kuwa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, nafasi yake imechukuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera aliyepandishwa cheo.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Makalla alisema, “nitazungumza nikifika, kwa sasa nipo njiani natoka Dodoma naelekea Katavi kukabidhi ofisi.”

Dalili za Makalla kuondolewa katika nafasi hiyo zilionekana baada ya Rais John Magufuli kumtaja katika moja ya ziara zake mkoani Mbeya.Aprili 27. Alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Sabasaba wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Rais Magufuli aligusia utendaji kazi wa Makalla.

Miongoni mwa mambo aliyozungumza ni sababu za kumuondoa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa kuwa ni kuchoma mazao ya wananchi akihusisha tukio hilo na kumhamisha Makalla kutoka Mkoa wa Mbeya na kumpelaka Katavi.

“Yalikuwa mambo ya ajabu sana, nikamwambia mkuu wa mkoa (Makalla) lakini nikaona na yeye anafanya mambo kidogokidogo nikaona ngoja nimtoe Mbeya nimpeleke Katavi kwa uangalizi zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Kwa kauli hiyo kuwa yupo kwenye uangalizi, pengine lilipaswa kumuamsha mbunge huyo wa zamani wa Mvomero kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo juzi usiku.

Aidha, kitendo cha Mkoa wa Katavi kushika nafasi ya mwisho katika kugawa vitambulisho vya wajasiriamali kinaweza kuwa kimemaliza hali ya ‘chini ya uangalizi’ na hivyo kumtoa nje ya ulingo Makalla, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2015.

Aprili Mosi, Rais Magufuli alipokuwa kwenye hafla ya kuwaapisha naibu katibu mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia sera, Adolf Ndunguru na naibu kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbipo alizungumzia kutopata ripoti ya vitambulisho vya Machinga.

Alisema tangu Desemba 10, 2018 alipotoa vitambulisho 67,000 kwa wafanyabiashara wadogo maarufu ‘wamachinga’ hakuna mkuu wa mkoa aliyewasilisha ripoti kuhusu mwenendo wa mchakato huo.

“Lakini hadi leo sijapata ripoti yoyote inayoonyesha mkoa au wilaya iliyomaliza kugawa vitambulisho vyake na kimekusanywa kiasi gani cha fedha na kupelekwa TRA. Ungekuwa umeshaniletea ningeshajua ni mkuu wa mkoa gani hataki kufuata maagizo nimtoe au wilaya gani imekaa navyo,” alisema Rais Magufuli.

Katika orodha ya vitambulisho vilivyogawiwa kwa wamachinga inaonekana Mkoa wa Katavi ulikabidhiwa vitambulisho 60,000 lakini vilivyogawiwa kwa wamachinga ni 3,370 hivyo kuufanya kuwa wa mwisho kwa kugawa vitambulisho hivyo ukiwa na asilimia 5.62 tu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa kabla ya kupitia tathmini ya ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wajasiriamali, aliitaja mikoa mingine iliyofanya vibaya na asilimia zake kwenye kuwa mabano kuwa ni Njombe (asilimia 11.14), Rukwa (asilimia 25.03), Iringa(asilimia 30.74) na Lindi (asilimia 33.58).

Kwa kauli hiyo na mwenendo wa ugawaji wa vitambulisho hivyo kwenye Mkoa wa Katavi, ilionyesha makala anaweza kuwa miongoni mwa aliosema atawaondoa kwa kutofuata maagizo yake.

Advertisement