Makinda avinyooshe kidole vyama vya siasa

Spika wa bunge mstaafu, Anna Makinda

Muktasari:

Spika wa bunge mstaafu, Anna Makinda amevitaka vyama vya siasa kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake ili nao washiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi ndani na nje ya vyama hivyo.

Dar es Salaam. Spika wa bunge mstaafu, Anna Makinda amesema kamati kuu za vyama vingi vya siasa zina wajumbe wengi wanaume jambo linalowafanya wasiwape wanawake nafasi za kugombea nafasi za uongozi.

Makinda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano uliowakutanisha wadau wa masuala ya wanawake katika kujadili namna ya kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Amesema tatizo la kukosekana kwa wanawake wengi hasa bungeni kunaanzia kwenye vyama vya siasa ambavyo kamati kuu zake zinapitisha majina ya wanaume wengi kwa kuhofia kupoteza kwenye majimbo.

“Wakati mwingine wanasema tukimweka mwanamke tutapoteza. Lakini wanatakiwa kutambua kwamba wanawake wana uwezo mkubwa wakipewa nafasi na tunashuhudia walio kwenye nafasi za uongozi wameacha alama kwenye nafasi zao,” amesema Makinda.

Spika huyo wa bunge la 10 amewataka wanawake pia kujiamini kwamba wanaweza na kuonyesha uwezo wao pale wanapopewa nafasi. Amesisitiza kwamba siasa ni hesabu, hivyo wanawake wajipange vizuri wanapotaka kugombea nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa chama cha wanasheria wanawake nchini (Tawla), Tike Mwambipile amesema wamebaini kwamba ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi bado ni mdogo, hivyo wamejipanga kuwahamasisha ili kuongeza ushiriki wao.

“Wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi hasa linapokuja suala la kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi. Wakati mwingine wanawake tuna matatizo yetu lakini mfumo dume ndiyo umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya jamii,” amesema Mwambipile.

Mbunge wa Hanang, Mary Nagu amesema suala la uongozi kwa wanawake liko kwao wenyewe hivyo wanatakiwa wajiamini na wawe na mikakati ya kufikia malengo yao. Amewataka wajue sifa zao na namna ya kuzielezea kwa watu ili wakubalike.