Mambo manne yatikisa wiki ya tisa ya Bunge

Dodoma. Wakati wiki ya tisa ya Bunge la Bajeti la mwaka wa 2019/20 ikimalizika, hoja nne kubwa zilizoibuliwa ndani ya vikao hivyo vitano ikiwamo ya Sh1.42 trilioni kati ya Sh2.142 trilioni za bajeti ya Wizara ya Nishati kuelekezwa katika mradi wa kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge.

Wiki ya nane wizara nne ziliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao kwa mwaka wa fedha 2019/20 na kupitishwa na wabunge ambazo ni Wizara ya Madini, Nishati, Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, kunafanya kubakia wizara moja ya Fedha na Mipango kabla ya bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/20.

Hoja nyingine zilizoibuliwa katika vikao hivyo vitano ni Uraia pacha; umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuruka vijiji na vitongoji na migogoro ya ardhi.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akiwasilisha hotuba yake alisema miradi mingine ni kusambaza umeme vijijini (Rea III) ambayo imetengewa Sh363.11 bilioni na mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi 1 Extension Mv 185 utakaogharimu Sh60 bilioni.

Maulid Mtulia (Kinondoni-CCM) alisema kwa kiasi kikubwa cha fedha hizo kinakwenda katika uzalishaji wa umeme kwa njia ya maji mto Rufiji ambao unagharama nafuu.

Mtulia alisema mafanikio katika mradi wa Stieglers Gorge utawezesha kupungua kwa gharama za uzalishaji hivyo kuwezesha kumudu ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

“Kuzalisha umeme kwa gharama nafuu kutawezesha kuanzishwa kwa viwanda vingi, hivyo watu wengi watapata ajira,” alisema Mtulia.

Uraia pacha

Hoja uraia pacha ambayo iligonga mwamba kwa mara nyingine baada ya mvutano wa wabunge wenyewe kwa wenyewe na Serikali iliibuliwa na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini-Chadema).

Akijibu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Damas Ndumbaro alisema suala hilo si la kutolea majibu ya haraka haraka, linahitaji mjadala wa pande zote, wabunge wa upinzani, CCM na Serikali.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe alisema uraia pacha si jambo geni duniani, nchi mbalimbali zimeruhusu aina hiyo kutokana na faida mbalimbali ambazo zinapatikana kwa mtu kuwa na uraia pacha.

“Faida ya Mtanzania ambaye ana uraia wa nchi mbili inawezekana akapata mitaji kule aliko kwa sababu ni raia anaweza kuleta kuwekeza huku lakini Mtanzania ambaye anaishi Marekani ana uraia wa Tanzania pekee si rahisi kupata hiyo mitaji,” alisema.

Migogoro ya ardhi

Hoja nyingine ni agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi la kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema migogoro ya ardhi imechukua muda mrefu kutatuliwa.

“Tangu nimeingia bungeni mwaka 2015 nimekuwa nikisikia wabunge wakilalamika kila siku, jitihada za kumaliza hiyo migogoro imekuwa ni changamoto jambo linaloonyesha hakuna nguvu kubwa eneo hilo,” alisema Peneza na kuongeza:

“Kazi yote inayofanywa sasa ni kama unaangaliwa uchaguzi, jambo ambalo si sawa. Kama ni ufanyaji kazi unatakiwa uwe mapema matatizo ya watu yatatuliwe mapema si kwa ajili ya uchaguzi.”

Umeme kuruka vijiji

Hoja nyingine ambayo ilisemwa na wabunge wengi wakichangia bajeti ya Nishati ni kurukwa vijiji au vitongoji.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akijibu hoja hiyo alisema wameyasikia mawazo ya wabunge na wanahitaji kuyafanyia kazi ili kuunganishia vijiji vyote.

Mbunge wa Bunda (Chadema), Easter Bulaya alisema kuna changamoto kubwa miradi kuchelewa, kuruka vijiji na kukosekana kwa umakini.

“Unakuta umeme wanaweza kuweka kwenye kijiji tu labda ni kitongoji kimoja, unakuta vingine havina umeme,” alisema Bulaya.