Mbowe, Matiko watimiza miezi miwili mahabusu, safari bado

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko jana walitimiza miezi miwili wakiwa mahabusu baada ya kufutiwa dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018.

Dar es Salaam. Jana mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walitimiza miezi miwili wakiwa mahabusu baada ya kufutiwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Licha ya hatua mbalimbali walizochukua baada ya kufutiwa dhamana kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanarejea uraiani, bado hatima yao kuhusu suala hilo imebaki kuwa kitendawili.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai na Matiko walifutiwa dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018, baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo wao pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho.

Kufuatia uamuzi huo, walikata rufaa Mahakama Kuu siku hiyohiyo wakipinga kufutiwa dhamana chini ya hati ya dharura, wakilenga kuishawishi mahakama isikilize rufaa yao na kuamuriwa haraka ili kujua hatima yao mapema. Hata hivyo, usikilizwaji wa rufaa hiyo ulikwama baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kukata rufaa Mahakama ya Rufani.

DDP alipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuisikiliza rufaa hiyo licha ya kuiwekea pingamizi la awali akitaka rufaa hiyo itupiliwe mbali. Ingawa tayari Mahakama ya Rufani imeshapanga tarehe ya usikilizwaji wa rufaa yao, lakini hatima yao bado haijajulikana kuwa itakuwa lini, kutokana na taratibu na hatua ambazo wanapaswa kuzipitia mpaka kufikia ama kurudi uraiani au kuendelea kusota mahabusu.

Mahakama ya Rufani imepanga kusikiliza rufaa ya Serikali, Februari 18. Hata hivyo baada ya kukamilika usikilizwaji wa rufaa siku hiyo wataendelea kukaa mahabusu wakisubiri tarehe ya uamuzi.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani ndio utakaotoa mwelekeo wa hatima yao.

Serikali katika rufaa yake imewasilisha jumla ya sababu tatu. Katika sababu ya kwanza, DPP anadai kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kwenye uamuzi wa kuamua kusikiliza rufaa ya kina Mbowe, kinyume cha kifungu cha kifungu cha 362 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Katika sababu ya pili, mkurugenzi huyo anadai Jaji alikosea katika uamuzi wake kwa kuamua kusikiliza rufaa hiyo kinyume cha kifungu cha 362(1) na cha 365(1) vya sheria hiyo.

Sababu ya tatu ni kuwa jaji huyo alikosea kwa kutomwezesha kupata haki ya kutosha ya kusikilizwa.

Iwapo Mahakama ya Rufani itakubaliana na hoja za rufaa ya DPP, itatengua uamuzi wa Mahakama Kuu (kuamua kusikiliza rufaa hiyo ya kina Mbowe) na hivyo rufaa hiyo ya kina Mbowe Mahakama Kuu itakuwa imekufa.

Hii maana yake ni kwamba Mbowe na Matiko wataendelea kuishi mahabusu hadi pale kesi yao ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itakapotolewa hukumu.

Endapo Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake itazikataa hoja za rufaa ya DPP na ikakubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu (kuendelea na usikilizwaji wa rufaa yao), itaamuru Mahakama Kuu iendelee na usikilizwaji huo.

Hivyo wanasiasa hao watasubiri wapangiwe tarehe ya usikilizwaji na baada ya usikilizwaji wa rufaa yao hiyo, kisha itatoa uamuzi.

Kama katika uamuzi wake huo Mahakama Kuu itakubaliana na hoja zao kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana, basi inaweza kuwarejeshea dhamana yao huku wakisubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi.

Hata hivyo, bado DPP anaweza akakata tena rufaa kupinga uamuzi huo kama hataridhika nao, lakini wakati huo tayari watakuwa wako nje. Lakini ikiwa Mahakama Kuu itatupilia mbali hoja zao za kupinga kufutiwa dhamana na ikakubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwa ilikuwa sahihi kuwafutia dhamana, basi wataendelea kuishi mahabusu hadi kesi yao ya msingi itakapoamuriwa.

Hata hivyo, wanaweza kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

Hivyo, bado Mbowe na Matiko wana safari yenye vikwazo hadi kufikia hatima yao, ambayo hadi sasa haijulikani kuwa itakuwaje.

Katika kesi ya msingi, Mbowe, Matiko na wenzao saba wakiwemo wabunge watano na viongozi wa chama wawili wanakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka 13 yakiwamo ya uchochezi na uchochezi wa uasi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondon wakati wakihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni.

Washtakiwa wengine ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; naibu makatibu wakuu (Bara), John Mnyika na Salum Mwalimu (Zanzibar), mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Tarime Vijijini, John Henche na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.