Mbowe aipongeza JWTZ kwa kuiunganisha Tanzania

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe amelishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa kiunganishi cha Taifa na kuendeleza umoja

Hai. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe amelishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa kiunganishi cha Taifa na kuendeleza umoja.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 2, 2019 wakati akitoa shukrani baada ya mazishi ya kaka yake, Meja Jenerali mstaafu, Alfred Mbowe.

“Jeshi limekuwa msaada mkubwa kwetu, limelia na sisi na halijatubagua kwa namna yoyote, naliomba liendelee kuwa kiunganishi kwa Taifa hili na litusaidie tuendelee kuwa wamoja,” amesema Mbowe.

Katika shukrani hizo, Mbowe amesema alitegemea kuwaona viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzia Wilaya ya Hai hadi Taifa katika msiba huo kutokana na kaka yake kuwa kiongozi wa Taifa.

"Kule Dar  es Salaam Rais wetu (John Magufuli) alikuja kwa niaba ya Serikali na sisi tumepokea watu wa makundi mbalimbali wamekuja kututembelea na kutupa pole, na ndugu zetu wa CCM nitawaita watani wangu hawa hawajaja tukawakataza, kwa hiyo waliokuwa hapa wanachama wa Chadema wamekuja kwa mapenzi mema kumsindikiza mwenyekiti wao.”

"Lakini ukweli kama ulivyoongea Mkuu wetu wa Mkoa (wa Kilimanjaro, Anna Mghwira) misiba ni mambo ya kutuunganisha wala si mambo ya kutufarakanisha. Ni dhahiri kwa nafasi aliyokuwa nayo kaka, Rais (Maguufuli) alitambua uzito huo na umuhimu na ndio maana alikuja kutufariji pamoja na Spika (Job Ndugai) na mawaziri kadhaa waliopo na waliostaafu,” amesema Mbowe.

Mbowe alitoa kauli hiyo baada ya Mghwira kuwapongeza Chadema kubeba msiba huo kama wa kwao licha ya kuwa ni msiba wa kitaifa.

Meja Jenerali Mbowe alizaliwa Januari 1952, alijiunga na JWTZ mwaka 1973 na kustaafu utumishi jeshini mwaka 2009.