Mbunge Chadema aitaka Serikali ya Tanzania kupunguza Paye, kuongeza mshahara

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ruth Mollel ameishauri Serikali ya Tanzania kupunguza kodi ya mshahara (Paye) ili kuwapa unafuu wa maisha watumishi wa umma ambao kwa miaka mitatu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, Novemba 5, 2015 hawajapandishiwa mshahara.

Dodoma. Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Ruth Mollel ameitaka Serikali ya Tanzania kupunguza kodi ya mshahara (Paye) na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ili waweze kwenda sambamba na kupanda kwa gharama za maisha.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa utumishi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 18, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

“Miaka mitatu hakuna nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma. Kiroba kidogo cha unga kilichokuwa kikiuzwa Sh2,000 hivi sasa ni Sh6,000 lakini mshahara ni ule ule wakati mnajua wazi kuwa watumishi wa umma ndio walipa kodi wazuri.”

“Ninasikitika maana watumishi ndio injini ya serikali leo wakigoma hakuna kitakachoendelea kwa nini Serikali haioni umuhimu wa watumishi na kufanya maisha yao kuwa rahisi. Paye ipunguzwe maana watumishi hao hao wanaoidai Serikali Sh61 bilioni hawajalipwa ila wao wakiwa wanadaiwa wanakatwa kwenye mishahara,” amesema Mollel.

Ili kuondokana na malimbikizo ya madeni, Mollel amesema Sh600 bilioni zilizotengwa kulipa madeni yaliyohakikiwa zilipwe kwa wakati na kuitaka Serikali kutafuta wataalam kupitia mfumo wa ulipaji ili kubaini sababu za madeni kutolipwa.