Mchuano ‘mawaziri wa fedha’ bungeni

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (kushoto) akizungumza bungeni jijini Dodoma juzi kuhusu hoja ya Zanzibar kukopa moja moja bila ya kuomba kibali kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji kwamba Zanzibar ikikopa, inayolipa ni Serikali ya Tanzania Bara yalimduwaza waziri wa zamani katika wizara hiyo, Dk Saada Mkuya.

Juzi jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Sh36bilioni ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2019/2020, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alishika shilingi akitaka Serikali itamke ni lini itapeleka bungeni muswada wa kubadilisha Katiba na sheria ili Zanzibar iruhusiwe kukopa na kuendesha miradi yake mikubwa kama ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege.

Katika maelezo yake, Dk Kijaji alisema, “Namuomba Kubenea aiachie shilingi. Dhamira ya Serikali ni njema kuhakikisha miradi yote mikubwa inatekelezwa pande zote mbili za Muungano.”

Kuhusu mkopo alisema, “Hili ni jambo la kikatiba, mchakato wake umeanza na yapo mambo tunajadiliana … tunapoomba Zanzibar ikope moja kwa moja nani wa kulipa mkopo huo? Nani wa kulipa hili ni jambo la Muungano. Serikali mbili zinakaa na kujadiliana.”

Wakati Dk Kijaji akitoa maelezo hayo, Dk Mkuya alionekana kushika kichwa kwa mikono yake miwili huku akiinama, kuangalia huku na huko na wakati mwingine kuziba mdomo ikiwa ni ishara ya kutokubaliana naye na alipoulizwa na mwandishi wetu nje ya viwanja vya Bunge sababu za mshangao wake alisema, “hicho kitu (Zanzibar kukopa) hakipo. Kila kitu kimewekwa vizuri katika sheria tunapokopa… Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikilipa maana yake Zanzibar imelipa.”

Mbunge huyo wa Welezo (CCM), aliendelea, “ndio maana mimi nimemshangaa sana waziri, tukiwa tunatoa kauli ambazo zina mkanganyiko huko wanaotusikia nao wanapata mchanganyiko.”

Hoja hiyo ya Kubenea pia ilichangia na Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almasi Maige ambaye alisema, “Hata siku moja, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijakataliwa inapotaka kukopa nje, inatoa taarifa kwa Serikali ya Muungano maana suala la fedha ni la Muungano. Wanaokopesha Zanzibar wanataka dhamana ya Serikali ya Muungano, si Serikali ya Zanzibar na hiyo inafanya Serikali ya Muungano kusajili madeni ya Zanzibar.”

Kadhalika, Mbunge wa Iramba Magharibi Dk Mwigulu Nchemba ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha alisema, “hili jambo tunaloliongelea ni la kikatiba na kiuchumi, kwenye sehemu ya kikatiba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Profesa Adelardus Kilangi) amesema marekebisho yake yanahitaji kushughulikiwa kikatiba kwa maana hiyo kama ni kikatiba, lazima lichukue muda na kufanyiwa kazi kwa uangalifu.”

Aliendelea, “ukirudi upande wa kiuchumi, wanaochangia hapa waelewe kwamba jambo la kukopa liliwekwa sehemu moja kwa sababu ulipaji unafanyika sehemu moja.” Alisema huwezi kufungulia ukopaji na mlipaji akawa mwingine, lazima anayelipa atazame kama makusanyo yake yanaruhusu kukopa mkopo katika Taifa husika.

Kuhusu kauli za wabunge hao, Dk Mkuya alisema, “niliona jibu lilikuwa rahisi na hakuwa peke yake (Dk Kijaji), hata Dk Mwigulu na Almasi Maige walisema kama alivyotamka Dk Kijaji, tena lilianzia kwa Maige ambaye alisema Zanzibar inakopa inatoa taarifa tu Tanzania Bara, si kweli. Katiba inasema itakopa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar haijawahi kukopa kutokana na masharti ya kikatiba na sheria yetu ya mikopo, misaada na dhamana ya mwaka 1974.”

Hata hivyo, Dk Mkuya alipata wa kuungana naye. “Nadhani hata Chenge (Andrew, mbunge wa Bariadi Magharibi) alilitolea ufafanuzi vizuri… Dk Kijaji alizungumza kwamba unapokopa inayolipa ni Serikali ya Tanzania Bara hakuna kitu kama hicho popote,” alisema Dk Mkuya, “wanaotusikia hususan vijana wetu wa Zanzibar wanashangaa. Inayokopa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo Zanzibar ni sehemu yake.”

Katika maelezo yake, Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema, “naomba tuweke rekodi sawa. Nadhani Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ameteleza tu ulimi. Dhamana inatolewa kwa mujibu wa Katiba na sheria ya mikopo, dhamana pamoja na misaada ya mwaka 1974 ambayo juzi tumeifanyia marekebisho hapa. Dhamana hiyo inatolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatuna Serikali ya Bara. Nimeona tunyooshe hilo kwa sababu ni suala la msingi sana,” alisema Chenge.