‘Mfalme Ruge’ alivyoitikisa Dar

Saturday March 2 2019

Msafara wa marehemu Ruge Mutahaba ukiwa eneo la

Msafara wa marehemu Ruge Mutahaba ukiwa eneo la Bamaga jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sasa unaweza kumwita “Mfalme Ruge”. Ni kutokana na jinsi umati wa watu ulivyojitokeza katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kushuhudia gari lililobeba mwili wake likipita kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuelekea Hospitali ya Lugalo ulivyopokewa jijini Dar es Salaam.

Ruge hakuwa mwanasiasa wala kiongozi wa Serikali ambaye angeweza kuvuta umati mkubwa barabarani kwa ajili ya kumpokea, lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa wakati wa mapokezi ya mwili wake jana, ni dhahiri anastahili sifa ya kuwa na cheo kipya hata kama sasa hayupo duniani.

“Rugee, Rugee,” waliiamba vijana waliokuwa wakikimbia sambamba na gari lililobeba mwili wake.

Wengine walionekana pembezoni mwa barabara wakiwa na mabango yameandikwa “Ruge aicon wa mapinduzi Tanzania”. “Ruge Shujaa”.

Msafara ulisimamishwa mara nne katika maeneo tofauti na watu walijazana barabarani wakitaka kutoa heshima zao kwake. Mara ya kwanza ulisimamishwa eneo la Kigogo, Tandale na Bamaga.

Ruge, mtu aliyejitoa maisha yake kukuza sanaa, kuinua wasanii, kuzindua fikra za vijana, kusaidia wajasiriamali na kushiriki shughuli nyingine za kijamii, alifariki mapema wiki hii akiwa hospitalini nchini Afrika Kusini baada ya kuugua kwa takriban miezi minne.

Advertisement

Mwili wa Ruge, ambaye anajulikana kwa wengi kutokana na kuwa mstari wa mbele katika burudani na kampeni ya Fursa alizofanya miaka ya karibuni, uliwasili jana na utaagwa leo kwenye viwanja vya Karimjee kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Bukoba mkoani Kagera ambako utazikwa Jumatatu.

Jana, picha za televisheni zilionyesha umati wa watu waliokuwa wamesimama barabarani, wengine kulisogelea gari huku wakionekana kutoa machozi na wengine kukimbia sambamba na gari lililobeba mwili huo.

Wakati fulani, gari hilo ambalo liliongoza msafara mrefu wa magari mengine pamoja na pikipiki, lilisimama na watu wakalisogelea na kulishika juu kama ishara ya kumuaga ‘Bosi’ Ruge, ambaye alikuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG), inayomiliki vituo vya televisheni, redio na kurasa za mitandao ya kijamii.

Baadhi walikuwa wakichungulia ndani kujaribu kuona jeneza lililobeba mwili wa Ruge, ingawa ilikuwa vigumu kutokana na vioo vya gari hilo kuwekewa pazia.

Vijana waliokuwa wakikimbia pembeni na nyuma ya gari hilo walionekana wakiweka mkono wa kulia kwenye komo la kichwa, ikiwa ni saluti kuonyesha heshima kwa kinara huyo wa burudani aliyeshiriki kubuni na kuandaa tamasha maarufu la Fiesta linalofanyika kila mwaka katika mikoa tofauti.

Mmoja wa watu waliokuwa wakiukimbiza msafara akiwa nyuma ya pikipiki, Jimmy Chiduo alisema ametoka mkoani Morogoro kwa ajili ya kumuaga Ruge.

Alisema amehuzunika kwani alimfahamu alipokwenda kwenye semina ya fursa mkoani humo mwaka juzi na tangu hapo amekuwa akimfuatilia na kuvutiwa na kazi zake.

Wakati umati wa vijana wakikimbia kufuata msafara huo wa magari na pikipiki, ofisi za CMG pia zilijaa watu wengine ambao walikuwa wakiusubiri mwili kwa ajili ya kuufanyia sala kabla ya kupelekwa Hospitali ya Lugalo kuhifadhiwa.

Mwanamke aliyekuwa na mtoto mgongoni alisema ametoka nyumbani kwake maeneo ya Tandale kwa Mtogole kwa ajili ya kumuaga Ruge na kwamba alimfahamu kupitia kampeni za Malkia wa Nguvu zinazowatunza wanawake waliofanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali.

Miezi mitano tangu alipokanyaga viunga vya ofisi za Clouds, Ruge jana aliingizwa akiwa amebebwa ndani ya jeneza.

Wafanyakazi walianguka vilio baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa CMG, Joseph Kusaga kusema kuwa wamempa heshima ya kuiona ofisi yake kwa mara ya mwisho.

Advertisement