Mpango: Watanzania acheni kujiita maskini

Muktasari:

  • Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango amesema Tanzania ni nchi tajiri na Watanzania hawana sababu ya kujiita maskini

Rungwe. Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango amesema Tanzania ni nchi tajiri na Watanzania hawana sababu ya kujiita maskini kutokana na utajiri ulion dani ya nchi, isipokuwa inahitaji mambo makuu matano kuvuna na kutumia rasilimali zilizopo.

Dk Mpango amesema Watanzania ili waweze kuvuna rasilimali zilizopo kama vile ardhi, hewa nzuri na madini kuna hitaji mambo makuu ya kuyafanyia kazi ambayo ni utaalamu, mtaji, kuyafikia masoko ya kuuza bidhaa zinazotengenezwa nchini, kuunganisha masoko ya ndani na nje ya nchi na kuweka kipaumbe katika uwekezaji.

Alisema hayo juzi akiwa na waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia uwekezaji, Angela Kairuki na mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe baada ya kutembelea mashamba ya maparachichi ya wakulima na wawekezaji wa kigeni kwenye viwanda vya kusindika na kuzalisha zao hilo wilayani hapa.

Viongozi hao walifika wilayani Rungwe kwa lengo la kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kushughulikia na kutatua mgogoro wa wawekezaji wa maparachichi wa kampuni ya Kuza Africa Co. Ltd na Rungwe Avocado Company (RAC) iliyo chini ya Bodi ya Tanzania Tea Parkers Ltd uliotokana na masuala ya hisa baada ya wawekezaji hao kutengana na kila mmoja kuanzisha kampuni yake.

“Nchi hii ina utajiri mkubwa, hii si nchi maskini Mwenyezi Mungu alitupa kila kitu. Ukiangalia hii ardhi ya Rungwe halafu ukasema wananchi wake ni maskini! Hapana. Lakini ili tuweze kuvuna hii rasilimali ya ardhi, hewa nzuri, madini na kila kitu Mungu alichotupa tunahitaji utaalamu, mtaji, masoko ya ndani na nje,” alisema.

Naye Kairuki alisema Serikali haipo tayari kuona inawapoteza wawezekezaji kwani ni msaada mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Alisema Tanzania kwa sasa ipo chini kwa asilimia 30 ya uzalishaji wa mbegu za mazao na asilimia 70 zinaagizwa kutoka nje ya nchi, lakini baada ya kufika kwenye mashamba ya wawekezaji hao wamefurahi kuona zaidi ya miche milioni moja kwa wilaya ya Rungwe pekee inatokana na maparachichi.