‘Mpango wa Serikali ni kubangua korosho yote inayonunua kwa wakulima’

Saturday November 24 2018

 

By Luis Kolumbia, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchweishaija amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha korosho yote itakayonunuliwa kwa wakulima inabanguliwa hapa nchini.

Tayari Serikali imeanza kununua korosho kutoka kwa wakulima baada ya agizo la Rais John Magufuli na kiasi kinachotarajiwa kununuliwa msimu huu ni tani 210,000.

Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Buchweishaija alisema hakuna korosho ghafi itakayosafirishwa kwenda nje ya nchi na kwamba kazi hiyo itafanyika hapa nchini.

Alisema Serikali imeliagiza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (Tirdo) kufanya tathmini na kubainisha mahitaji ambayo yatafanikisha ubanguaji wa korosho kufanyika nchini.

Alisema wataalamu hao wataangalia mahitaji ya kufufua kiwanda cha Buko ambacho sasa kiko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Alisema Serikali inafikiria kuvichukua viwanda vingine 10 ambavyo mwenendo wake sio mzuri tangu vibinafsishwe, “Tupo katika mazungumzo na wamiliki binafsi wa viwanda ili kuona ni tunavyoweza kushirikiana nao katika kubangua korosho. Baada ya kukamilika kwa mazungumzo tutaingia nao mkataba,” alisema.

“Hatutaki kuona viwanda vikifa au vikisitisha uzalishaji kwa sababu ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ukuaji wake na kulinda ajira za Watanzania.”

Kadhalika, Profesa Buchweshaija alisema Serikali inazo fedha za kutosha kununua korosho zote huku akipinga madai ya kwamba kasi ndogo ya ununuzi wa korosho inatokana na uhaba wa fedha.

“Upinzani utaendelea kuwapo lakini Serikali imedhamiria kuhakikisha wakulima wananufaika, ndiyo maana tuko makini na kujiridhisha na orodha ya wakulima,” alisema.


Advertisement