Msuya aelezea machungu viwanda vilivyobinafsishwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu mstaafu amezungumzia namna alivyopambana wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere kusuka mtandao wa viwanda nchini, lakini vingi vikaja kubinafsishwa kwa bei ya kutupwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya ameelezea machungu yake jinsi viwanda vikubwa alivyosimamia kuvijenga enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere vilivyobinafsishwa kwa bei ya kutupa huku akizungumzia matumaini kuwa mageuzi yanayofanywa na Rais John Magufuli yatairudisha Tanzania kwenye mstari.

Akizungumza katika kipindi cha Hamza Kassongo on Sunday kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Msuya alieleza kuwa pamoja na mambo mengine, ushawishi walioufanya kipindi hicho kupata fedha za kujenga viwanda na kuelezea mpango wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma kuwa kosa kubwa linaloigharimu Tanzania.

Aliyasema hayo kwenye mahojiano maalumu kuhusu miaka 57 Uhuru wa Tanzania.

Alianza kufanya kazi katika kabla ya uhuru kama mtumishi mwandamizi katika Serikali ya mkoloni katika idara ya maendeleo ya jamii.

Mwaka 1972 aliteuliwa kuwa mbunge na waziri wa fedha akiwa na miaka minne. Baadaye mwaka 1975 Nyerere alimteua tena mbunge na kumpa wizara ya viwanda na maelekezo maalumu kuhakikisha kuwa Tanzania inaanza kuzalisha vitu vyote ambavyo Kenya waliitumia Tanzania kama soko.

Mwalimu Nyerere alimpa maelekezo kuwa kama asingeweza hilo walau achepushe biashara Tanzania iliyofanya na Kenya na kupeleka kwingine baada ya uhusiano kudorora.

Msuya anasifika kwa kusimamia ujenzi wa viwanda vikubwa vya kwanza vya saruji, nguo na kuweka mfumo mpana zaidi wa viwanda.

“Mahali pengine yalifanyika makosa katika ile privatisation (ubinafsishaji). Watu wakiniuliza nasema tulifanya makosa. Unachukua mtu ambaye hajaendesha kiwanda unampa kiwanda, yeye nia yake ni kwamba atarudisha ile pesa yake, auze majengo au mitambo apate pesa yake aende zake,” anasema.

Anasema tatizo la viwanda kufanya vibaya lilichangiwa sana na kukosa menejimenti zenye uzoefu na ubunifu katika kuendesha mashirika, akisema, “kule ambako tulibahatika kupata watu wenye uzoefu mkubwa, kwa mfano Breweries (viwanda vya bia) mpaka leo wanasifika.”

Msuya anasema Taifa lilipotea njia kuhusiana na sera nzima ya viwanda na uwekezaji pale walipoamua kuunda tume ya kusimamia uuzaji wa mashirika ya umma kwa watu na kampuni binafsi.

“Yale niliyosimamia mimi tulifuata mwelekeo tuliopewa na Baraza la Mawaziri. Sasa baada ya pale wakaunda tume moja ilikuwa inaitwa Parastatal Sector Reform Commission (anatikisa kichwa kwa masikitiko), kwa maoni yangu that is where things went wrong (pale ndipo tulipokosea).

Anasema, “Iikuja kitu kuhubiri kwamba state (Serikali) tulikosea kujihusisha na uwekezaji, kwa hiyo ikawa ni kuuza, uza, uza! Nafikiri kulikuwa na pressure (msukumo) kutoka World Bank (Benki ya Dunia) na wapi na wapi, na matokeo yake ndio hayo.”

Viwanda Morogoro

Msuya haelewi ni kwa nini viwanda vikubwa kama vya ngozi, Polyster na Canvas vilivyokuwa vya kimkakati katika kuinua uchumi wa nchi vilibinafsishwa na sasa havipo tena. “Let me tell you one thing (acha nikuambie jambo moja) ambalo baadhi yetu linatuuma. Pale Morogoro ule mji wote ulijengwa na Serikali kwa viwanda, kulikuwa na viwanda vya ngozi, kulikuwa na viwanda vya polyster, kulikuwa na kiwanda cha kutengeneza canvas,” anasema.

“Kulikuwa na kiwanda kikubwa cha ngozi ambacho kilikuwa kichukue ngozi zote, wakaamua kuuza, na wakaanza kuuza kwa yeyote aliyekuja, wengine wakauza ile mitambo wakaondoka, mie sidhani kuna bidhaa inatoka Morogoro kwenye kiwanda cha ngozi.”

Karatasi Mufindi

Msuya anaeleza pia masikitiko yake kwa nini Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi walichojenga kwa fedha nyingi siyo mali ya Watanzania tena.

Anasema, “Tulikuwa na kiwanda kikubwa tumejenga pale Mufindi ili kitumie ile miti iliyopandwa pale kama malighafi. Gharama ya kile kiwanda pamoja na miundombinu yake ilikuwa zaidi ya Dola za Kimarekani 300 milioni.”

“Kilifanyiwa uchambuzi na Benki ya Dunia na KFW na mabenki mengi wote wakakubali kwamba kinalipa. Tukawekeza pale, ulipokuja kubinafsisha wakauza kwa Singasinga mmoja huko Kenya. Nasikia bei waliyouzia ilikuwa ni kiduchu.”

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC)

Msuya anauelezea ubinafsishwaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuwa jambo ambalo halikuwa na tija kwa Taifa. “Ni painful (inauma) watu kama akina Amon Nsekela (aliyewahi kuwa ) walifanya kazi kubwa kuweka mtandao NBC iwe kila wilaya wananchi waweze kuweka fedha ili kuingia hatua ya pili ya kuwashawishi wakope, sasa kwa sababu zisizojulikana ikaamuliwa nayo iuzwe, ”anasema Msuya.

“Kwa hiyo tunadanganywa…vitu hivi vinataka roho ngumu na ujiamini, na ujue unataka kwenda wapi, matatizo mengine ni ya kawaida. Na mimi nimekuwa nikisema wapi tulikosea. Lazima tujifunze kuwa badala kusema tubinafsishe tungefanya walichofanya Wachina.”

“Unajua zamani nao walijifungia ndani, akaje yule mzee mfupi (hakumbuki jina) akafungua mlango, akasema tunakaribisha hewa iingie hapa ndani, wakaribisha makampuni ya Kijapani, Kingereza Kimarekani na Kijerumani waingie ubia na makampuni ya China watengeneze bidhaa wauze duniani kote.