Nandy sasa ni kujizawadia magari kwa kwenda mbele

Saturday November 17 2018

Msanii anayefanya vizuri kwa sasa katika muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu kama Nandy, amesema anatarajia kujizawadia magari mengine mawili mapema mwakani.

Msanii huyo alishangaza watu Novemba 9 mwaka huu alipojizawadia gari aina ya BMW X1 wakati wa hafla ya uzinduzi wa albamu yake ya African Princess iliyofanyika klabu ya usiku ya Next Door, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi, Nandy alieleza kuwa sababu ya kuamua kujizawadia gari hilo la kifahari ni kutokana na kuwa na ndoto ya kulimiliki tangu alipoingia kwenye muziki.

Msanii huyu ambaye kwa sasa anasumbua anga la muziki na wimbo Aibu, alikiri kwamba gari hilo alilijua baada ya kuingia kwenye muziki kwani kabla ya hapo alikuwa hajui magari.

“Tangu nimeingia kwenye muziki nimejua aina mbalimbali za magari tofauti na ilivyokuwa awali, na kati ya magari ambayo nimekuwa na ndoto ya kuyamiliki ni hili nililojizawadia na mengine mawili ambayo natarajia kujizawadia Februari mwakani Mungu akipenda kama mambo yangu yataenda sawa,” alisema msanii huyo.

Alitaja aina ya magari hayo mawili anayotarajia kujizawadia hiyo mwakani kuwa ni Audi 7 na Range Rover.

Kuhusu kujizawadia badala ya kuzawadiwa kama ilivyozoeleka kwa watu wengi, Nandy alisema kwamba kwake anaona anayekuzawadia anaweza asikupe lile hitaji la moyo wako na wakati mwingine itategemea na uwezo wake kifedha.

Hivyo kwake kujizawadia mkoko wake huo roho yake imekuwa burudani kwani ndio zawadi aliyoipenda na isitoshe imetokana na jasho lake.

Advertisement