Nchi nayo inahitaji kiki kama Diamond Platnumz?

Mdogo wangu Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ huwa hafichi hisia zake anapozungumzia biashara yake ya muziki. Siku moja aliweka wazi kwamba anapenda kuandikwa. Iwe kwa ubaya au uzuri. Inamuongezea idadi ya watu wanaomjua.

Wakati mwingine akiona watu hawamzungumzii sana basi anachukua fedha zake za kigeni ‘Dola’ ambazo zimepotea mjini, anaanza kujirekodi akizihesabu. Ukitukana hajali. Ukimpongeza kwa ‘utajiri’ wake pia hajali. Ili mradi siku imepita huku akizungumziwa.

Hiki kitendo cha jina lako kutajwatajwa kwa sababu zozote zile siku hizi vijana wa kizazi kipya wanaita ‘kiki’. Maisha yetu yamehamia mitandaoni. Yamekuwa magumu kwelikweli kwa watu wanaojitambua. Yamekuwa magumu pia kwa watu wa kizazi cha zamani. Hawaelewi kinachoendelea katika jamii yetu.

Majuzi ilipoanguka ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines) dakika chache baada ya kupaa kutoka katika uwanja wa Bole, nchini humo ndipo nilipogundua kwamba nchini mwetu idadi ya vichwa maji imeongezeka. Kuna tatizo mahala. Orodha ya marehemu kutoka nchi mbalimbali ilipotoka kuna wajinga wakaulizana. ‘ina maana hakuna Mtanzania aliyefariki kwa ajali hiyo?’. Mtu mzima na akili zake anauliza swali hili baada ya kusoma orodha ya nchi ambazo raia wake walihusika katika ajali hiyo.

Wengine wakaenda mbali zaidi. Kipuuzi tu wakamlaumu Namba Moja kwamba amebana sana kiasi kwamba watu hawasafiri na ndio maana hakuna abiria Mtanzania aliyefariki katika ajali hiyo. Ndiyo, tumefika hapa. Ina maana kuna watu walitaka kuona Mtanzania amefariki katika ajali ile ili mioyo yao iridhike?

Kwamba jina la nchi yetu linapaswa kuwepo kila mahali. Kwa mazuri na mabaya alimradi nchi inapata kiki. Kuna wazimu fulani umetawala nchini. Nadhani Watanzania wana msongo fulani hivi wa mawazo. Unapoanzia msongo huo sipajui, unapoishia ni pale unaposikia mtu mzima uliyemuamini anashangaa “yaani hakuna Mtanzania aliyefariki katika hii ajali?” Yaani tumefika hapa.

Hata hivyo, wakati mwingine sishangai sana. Unaweza kumkuta mtu anatabasamu baada ya kusoma kichwa fulani cha habari kinachosema ‘Tanzania miongoni mwa nchi saba zinazoongoza kwa kutupa uchafu barabarani’. Kuna kitu cha kufurahisha hapo au ili mradi nchi imetajwa?.