Ndugai aishauri Serikali kero ya mizani ya magari

Muktasari:

  • Ndugai amesema pamoja na nia nzuri ya Serikali kulinda barabara lakini wananchi wamekuwa wakipata kero kutokana na tofauti ya majibu ya vipimo licha ya kwamba vipimo vyote hivyo vinamilikiwa na Tanroads.

Dodoma. Si madereva wa malori tu, hata Spika Job Ndugai anakerwa na jinsi mizani ya magari makubwa inavyofanya kazi.

Kiongozi huyo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano anaona kero hizo zinaichafua Serikali na sasa anaitaka izitatue.

Mizani hiyo iliyo katika kila barabara inayotoka nje ya mikoa, hutumiwa kwa ajili ya kupima uzito wa magari kulingana na vigezo vya barabara, lakini madereva wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa udanganyifu unaosababisha mizani zionekane zinatoa matokeo tofauti ya vipimo kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.

Na jana, wakati wa semina ya Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC) iliyolenga kuangalia mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Uzito na Vipimo, Ndugai alibeba kilio hicho.

Alisema pamoja na malengo mazuri ya Serikali ya kulinda barabara, wananchi wamekuwa wakipata kero kutokana na tofauti hiyo ya majibu ya vipimo ambavyo alisema mmiliki wake ni mmoja, yaani Wakala wa Barabara (Tanroads).

Alitoa mfano wa malori zaidi ya 60 ya kampuni ya saruji ya Dangote ambayo hivi karibuni yalizuiwa na Tanroads mkoani Kigoma.

“Magari haya yametoka Mtwara yamepimwa uzito pale kiwandani, yametembea katika vipimo vyote (na yameonekana) yako sahihi, lakini yamefika kituo cha mwisho wanasema kuwa yamezidi uzito sijui kilo 30 sijui 50,” alisema Ndugai.

“Wameyazuia karibu magari 60 yasiingie Kigoma na Kigoma yenyewe haina cement (saruji) na mnajua Kigoma wanavyorusha bei (ya saruji).

“Hata logic (mantiki), hii si kampuni moja na hawa wa vipimo si vya kampuni moja? Iweje huku kote iwe sawasawa halafu cha mwisho ionekane tatizo?

Alisema tatizo hilo ni kwa magari mengine mengi, yakiwemo ya mafuta.

“Linatoka Kigamboni liko sawasawa linakuja Vigwaza liko sawasawa. Likifika Mikese unakuta limekamatwa wanalipa faini mafaini yenyewe ni makubwa,” alisema.

Alisema kama tatizo hilo lisipoangaliwa, athari zinazoweza kutokea ni pamoja na kupoteza wafanyabiashara wanaopitishia bidhaa ama kununua Tanzania.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alisema udanganyifu wa vipimo umekuwa ukichangiwa na wafanyabiashara wasio waadilifu na madalali wanaotaka kupata faida kubwa.

“Vipimo visivyo sahihi vimepachikwa majina mengi, kama kimbo, visado debe, plastiki na ndonya. Vipimo hivyo vyote vinafaa kupigwa vita kwa kuwa vinarudisha nyuma maendeleo ya sekta ya viwanda na kilimo,” alisema.

Mkurugenzi wa Wakala wa Vipimo (WMA), Dk Ludovick Manege alisema utafiti uliofanywa na kampuni tatu tofauti kwa zao la vitunguu mara baada ya operesheni lumbesa umeonyesha kipato cha wafanyabiashara wa kati kilipungua kwa asilimia saba na vitunguu kwa asilimia 12.

Katibu mkuu wa APNAC, Daniel Mtuka alisema hivi sasa wanaelekeza nguvu yao kwa Serikali kuhimiza Sheria ya Rushwa kuletwa upya bungeni ili kuondoa mambo wanayoona hayaendi sawa.

Alitolea mfano mlolongo mrefu wa kesi za rushwa kutokana na sheria kutaka faili kwenda kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kabla ya kwenda mahakamani.