MUUNGANO WA TANGANYIKA-ZANZIBAR 1964: Nyerere avunja ziara ya Kambona Tabora, Kigoma-9

Muktasari:

Katika toleo lililopita tuliona jinsi Balozi wa Marekani nchini Kenya, William Attwood, alipomshauri Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Tanganyika, Oscar Kambona, wakutane. Baada ya mazungumzo akamsisitiza akifika Dar es Salaam akutane na Balozi wa Marekani nchini Tanganyika, William Leonhart. Na wawili hao walipokutana Dar es Salaam, Kambona alionekana kushawishi na kuunganisha Zanzibar na Tanganyika na kwamba ampelekee wazo hilo Rais Julius Nyerere. Endelea…

Baada ya mazungumzo kati ya Balozi William Leonhart wa Marekani na Oscar Kambona aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, kazi ilikuwa ni kumshawishi Rais Julius Nyerere wa Tanganyika.

Wazo la muungano lilimsisimua Kambona, naye alitaka kumsisimua Nyerere.

Hayo yalitokea mchana wa Aprili 18, 1964—muda mfupi kabla Kambona hajaondoka mjini Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Tabora na Kigoma.

Kama Kambona alivyofikisha habari za mazungumzo yake na Balozi Leonhart kwa Nyerere, ndivyo Balozi Leonhart naye alivyoripoti mazungumzo yake na Kambona kwa Serikali ya Marekani.

Alipofika Ikulu siku hiyo mchana, Kambona alimpasha Nyerere habari za mkutano wake na Balozi Leonhart kuhusu uwezekano wa Tanganyika kuungana na Zanzibar.

Habari zinasema wakati fulani wazo hilo liligusa hisia za Nyerere, lakini sasa lilimwingia akilini zaidi kuliko awali. Alichotaka Nyerere tangu awali ni Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini alishindwa kushawishi litokee kwa sababu wenzake hawakuwa tayari.

Hata hivyo, suala la shirikisho la Afrika Mashariki lilimjia Nyerere kwa njia ya pendekezo pia. Kwa kuwa sasa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulionekana kuwezekana, aliona hiyo ndiyo njia ya kuwaonyesha Kenyatta na Obote kuwa uwezo anao. Hata hivyo alihitaji muda wa kutosha wa kulifikiria jambo hilo.

Siku iliyofuata, Mwalimu Nyerere alikaa ofisini kwake na baadhi tu ya watendaji wake akijaribu kuomba na kutoa ushauri.

Mama mmoja wa Kiingereza aliyekuwa akimsaidia, Joan Wickens, alikuwa na kazi ya kupekua kumbukumbu nyingi za aina ya shirikisho na muungano za nchi nyingine duniani.

Hapa ndipo Nyerere alipoonekana kuwa na shughuli nyingi. Huenda hapa ndipo alipokuwa akilifanyia kazi wazo alilopewa la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar. Kukuru kakara zikawa nyingi. Kile kilichokuwa kikiendelea katika akili yake kilimwambia kuwa siku mbili tatu zijazo zingekuwa na mambo mengi yaliyohitaji kushughulikiwa.

Kama alikuwa na wazo la Muungano mapema zaidi kabla ya mazungumzo ya Aprili 18 kati ya Kambona na Balozi Leonhart, hilo lingeonekana katika gazeti la Nationalist and Freedom katika toleo lake la kwanza, au la pili, au asingehangaika kumtuma Kambona kwenda ziarani Tabora na Kigoma na kisha alazimike kumtaka avunje ziara hiyo na arudi tena Dar es Salaam mara moja kwa ajili ya kazi hiyo maalumu.

Hangekuwa na haja ya kuitisha kikao cha dharura cha Bunge katika kipindi cha siku mbili tu. Na wala Bunge lisingekaa siku ya Jumamosi tofauti na ilivyo kawaida yake, na wala Muungano haungefanyika siku ya Jumapili kama ulivyofanyika, au angalau siku moja tu baada ya kikao cha dharura cha Bunge.

Baada ya wazo hilo kumkolea, ndipo alipoagiza Kambona avunje ziara yake ya kutembelea Kigoma na arejee Dar es Salaam “haraka iwezekanavyo”. Akiwa tayari amewasili Tabora akijiandaa kwenda Kigoma, Kambona alipata ujumbe na kuanza safari kurudi Dar es Salaam.

Kutokana na mazungumzo hayo, Wamarekani walimwagia Kambona sifa kwa sababu tu alionyesha wasiwasi fulani na kutishwa na athari za ukomunisti Zanzibar. Na pia walivutiwa naye kwa sababu waliona kuwa angalau, kwa kiasi fulani, angeweza kushiriki kuufutilia mbali ikiwa angepewa msukumo wa kufanya hivyo.

Kwa upande mwingine, kilichokuwa kimempata John Okello siku chache zilizopita—yaani kupigwa marufuku kurejea Zanzibar—kilikaribia kumpata Abdulrahman Babu. CIA ilikuwa imeweka mtego wa kumnasa asirudi Unguja. Lakini Carlucci, akiwa Zanzibar, aliitahadharisha CIA kwa kuionya kwamba “huenda mipango yetu ya maana ikavurugika kabla haijapevuka”.

Carlucci alituma ujumbe huo asubuhi, Jumapili ya Aprili 19, kwa majasusi waliokuwa Nairobi, Kenya, ambao nao waliupokea, wakaujadili katika vikao vya siri, na kisha wakautuma tena kwenda Marekani kuchanganuliwa zaidi.

Muda mfupi kabla ya wakati huo, Balozi Leonhart alituma taarifa kwenda Washington iliyosema: “Jambo linaloweza kutokea ni lile linalofanana na uvumi ulioenea mjini London (Uingereza) kwamba (Abdulrahman Mohammed) Babu hataruhusiwa kurejea tena Zanzibar. Zanzibar iliyotawaliwa na (Kassim) Hanga (Makamu wa Rais wa Zanzibar) na (Abdul Aziz) Twala (Waziri wa Fedha) haitakuwa na hali ya mambo inayonukia vizuri na inayowazika, lakini inawezekana kabisa kwamba Kambona anaweza kuomba msaada wowote, uwe ni wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja, kutoka kwetu kwa niaba ya Hanga, mapema wiki ijayo.”

Kwa mujibu wa ujumbe huo, ni rahisi kuona kuwa Kassim Hanga alikuwa ameandaliwa kwa ajili ya Zanzibar na mshirika wake mkubwa alikuwa Kambona.

Katika taarifa yake aliyoituma Marekani, Balozi Leonhart aliendelea kusema: “Huenda tukahitaji kufanya kazi harakaharaka bila kukawia. Jaribio lolote la kutaka kumuondoa Babu, (Salim) Rashid na mfuasi yeyote anayewatii watu hawa linaweza pia kuharakisha fujo zitakazolazimisha matumizi ya nguvu kutoka nje ya Zanzibar.”

Akijibu ujumbe huo wa simu, naibu katibu mkuu wa mambo ya Nje wa Marekani, George Wildman Ball, alisema: “Idara (CIA) inatoa baraka zake zote kwa kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na Tanganyika: Shirikisho la Tanganyika-Zanzibar au Muungano ... Mpaka kufikia hatua hii hatujapata ishara ya kuombwa msaada wowote ambao Marekani inatakiwa kuutoa. Na kama kuna (msaada) wowote unaohitajika, ambao Kambona anaweza kuuomba atakapokuja kukuona tena Aprili 20, ni vizuri tukajulishwa mapema tuweze kuuandaa.”

Itaendelea kesho