Odinga ashauri Afrika ijenge miundombinu kwa fedha zake

Friday March 22 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Umoja wa Afrika (AU) umezishauri nchi wanachama kutumia kwanza vyanzo vya ndani kujenga miundombinu msingi kabla ya kukopa fedha kutoka nje.

Ushauri huo uliotolewa jana na balozi wa AU anayeshughulikia masuala ya miundombinu ya usafiri na uchukuzi, Raila Odinga umekuja siku chache baada ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kusema Afrika inaweza kutatua changamoto ilizonazo kwa kutumia fedha za ndani.

Alikuwa akifunga mkutano wa siku mbili uliowakutanisha takriban wataalamu 30 wa sekta hiyo kutoka nchi wanachama wa AU.

Raila alisema endapo kutakuwa na mikakati makini, Afrika inaweza kuanza kutekeleza miradi ya kipaumbele kwa fedha za ndani na ikaenda kuongezea nje sehemu ndogo iliyobaki, hivyo kuepuka uwezekano wa kufilisika.

Alipendekeza kuitumia kwa umakini mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni na mashirika ya bima, benki za biashara za ndani pamoja na kuishirikisha sekta binafsi (PPP) ili kuwa na mawasiliano ya uhakika baina ya mataifa ya Afrika.

Bila kuzitaja, waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya alisema zipo baadhi ya nchi ambazo zimekopa mpaka zikafilisika, suala linalotakiwa kuepukwa wakati wa kufikiria ujenzi na upanuzi wa barabara kuu, madaraja, reli na bandari.

Msimamo wa Odinga unafanana na wa rais wa AfDB, Dk Akwinum Adesina alioutoa wiki iliyopita kwenye mkutano mkuu wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (Unea) uliofanyika jijini Nairobi kuhusu Afrika inavyoweza kukabiliana na changamoto za mazingira.

“Afrika inahitaji mfumo wake kukabiliana na mazingira, fedha zipo za kutosha isipokuwa namna ya kuzitumia,” alisema Adesina.

“Ukiziunganisha benki, mifuko ya hifadhi ya jamii, bima na taasisi nyingine za fedha, kuna zaidi ya dola 1.8 trilioni zinazotosha kukabili uchafuzi wa mazingira.”

Wataalamu wa miundombinu wamekutana jijini hapa kubainisha fursa kisha kupendekeza vyanzo vya mapato kwenye mkutano ulioandaliwa na Sekretarieti ya Programu ya Maendeleo Afrika (Nepad).

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Miliki za Ujenzi wa Wizara ya Ujenzi, Said Mndeme aliyemuwakilisha katibu mkuu wa wizara, alisema wametumia mkutano huo kumulika maeneo muhimu na kuweka mkakati wa kutatua changamoto zilizopo.

“Afrika ina nchi 55 hivi sasa, lakini 16 hazina bandari. Kati ya hizo, sita zinahudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuwepo kwa umuhimu wa kuliunganisha jiji hili na nchi jirani,” alisema Mndeme.

AU inakusudia kuiunganisha Afrika kuanzia Kaskazini mpaka Kusini na kutoka Mashariki hadi Magharibi kwa kujenga miradi ya kielelezo licha ya mipango iliyopo kwa kila ukanda huku Serikali zikiendelea na mipango ya ndani.

Mshauri mwandamizi wa ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Maendeleo wa AU (Auda-Nepad), Adama Deen alisema miaka michache ijayo Afrika itakuwa kitovu cha biashara, hivyo ni lazima iunganike.

“Tunahitaji miundombinu makini ya usafiri, usafirishaji na uchukuzi kufanikisha biashara na kukuza uchumi,” alisema Deen.

Advertisement