Breaking News

Ofisa elimu ataja dawa ya kumaliza ufaulu duni mkoani kwake

Friday July 12 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Musoma/Mwanza/Bukoba. Ofisa elimu Mkoa wa Mara, Emmanuel Kasongo ametangaza ‘kula weekend’ yake ya Jumamosi na Jumapili akitembelea shule tatu za mkoa huo zilizoshika nafasi tatu kati ya shule 10 za mwisho katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa jana Alhamisi Julai 11, 2019.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana Alhamisi Julai 11, 2019, muda mfupi baada ya matokeo hayo kutangazwa, Kasongo alisema matokeo hayo yameushtua viongozi wa idara ya elimu mkoa, kwa sababu hayakutarajiwa kutokana na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ya shule hizo.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde, shule tatu za mkoa wa Mara za Nyamunga, Buturi na Bumangi ni kati ya shule 10 zilizoshika nafasi ya mwisho.

Shule zingine za mwisho na mikoa inayotoka kwenye mabano ni Eckernforde (Tanga), Nsimbo (Katavi), Mondo (Dodoma) na Haile-Selassie, Tumekuja, Mpendae na Kyembesamaki ‘A’ Islamic zote za Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

“Shule za za Buturi na Bumangi ni kati ya shule zenye mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia na uongozi imara; kwa kweli sijui kilichotokea hadi zipate matokeo haya. Nitazitembelea kabla ya Jumatatu ikibidi nitafanya hivyo hata siku za Jumamosi na Jumapili,” amesema Kasongo.

Wakati uongozi wa elimu mkoa wa Mara ukikuna kichwa kutafuta sababu za shule tatu za mkoa huo kuwa kwenye orodha ya shule 10 za mwisho, Mkuu wa shule ya sekondari Nganza ya jijini Mwanza, Yasinta Lyimo na Mwalimu wa masomo ya biashara shuleni hapo, Zacharia Msonge wamejivunia shule yao kutoa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya saba Kitaifa kwa ufaulu katika masomo ya mchepuo wa biashara, na uchumi.

Advertisement

Wakizungumza kwa nyakati tofauti shuleni hapo jana, Lymo na Msonge wametaja usikivu, kufuata ratiba ya vipindi na kujisomea, nidhamu kwa wote na kumcha Mungu kuwa miongoni mwa sababu za mafanikio ya mwanafunzi, Irene Barakaeli ambaye ni kati ya wanafunzi 67 wa shule hiyo waliopata ufaulu wa daraja la kwanza.

Matokeo mengine ya wanafunzi hao ni wanafunzi 151 daraja la pili, 200 daraja la tatu, 13 daraja la nne na sifuri moja.  

 Imeandikwa na Beldina Nyakeke, Johari Shani na Phobias Bashaya

Advertisement