UCHOKOZI WA EDO: ‘Party One’ ya Mzee Membe na Rostam imenivuruga

WALE vijana wahuni wanaojiita Shilawadu huwa wana msemo wao fulani hivi umeanza kuwa maarufu. ‘mambo ni mengi muda ni mchache’. Ni kweli hawakukosea. Tanzania ya leo unahitaji kuwa na simu yenye bando muda wote. Vinginevyo unapitwa na habari. Unadhani ni mpya kumbe watu wamehamia kwingine.

Nilikuwa namtafakari mkuu wa mjengo pale Dodoma pamoja na yule kijana anayeitwa Masele. Nikaanza kutafakari kwa makini zaidi na zaidi. Nikachukua ‘Laptop’ yangu niwachokoze. Ghafla rafiki yangu wa karibu akanitumia video ya tajiri Rostam Aziz akiongea kitu.

Nikaweka ‘Laptop’ kando nikachukua simu na kumsikiliza Rostam. Unaachaje kumsikiliza tajiri aliyerudi ghafla katika anga za siasa? Mtu ambaye wakati fulani niliambiwa anatutengenezea ‘mabosi’ wetu hapa nchini.

Nikamsikiliza kwa makini. Alikuwa anampiga mkwara mtu mwingine mzito kama yeye. Mzee Membe. Tofauti yao ni kwamba huyu Rostam ni tajiri na mwanasiasa, Mzee Membe ni Mwanasiasa kamili. Mzee Rostam alikuwa anampiga mkwara Mzee Membe kwamba asijisumbue kugombea urais ndani ya chama chake kwa sababu taratibu za chama zinasema Namba Moja lazima agombee tena kupitia kiti hicho. Hata mimi huwa najua hivyo.

Hapo hapo nikawaza. Mbona Mzee Membe hajasema kwamba anagombea urais? Inawezekana Rostam anajua mengi zaidi yetu, lakini angekaa kimya tu. Kwa kufanya vile ni kama anampa ‘kiki’ isiyo na sababu Mzee Membe. Anamjenga. Au Rostam anamtangaza kijanja Membe kuwa mgombea? Mbona anamuweka hadharani mapema?

Siku moja baadae naye Mzee Membe akaibuka. Akajibu mapigo ya Mzee Rostam. Akaongea mafumbo ambayo sisi tulioishia darasa la saba tulifanikiwa kuelewa kiasi. Lakini cha ajabu ni kwamba hakutaka kukata mzizi wa fitina. Hakusema kwamba anagombea au hagombei. Aliishia kutupiga mafumbo tu. Akaondoka na ile suti yake ya kijivu huku akiwa amezungukwa na mabaunsa wake kama Diamond Platinumz. Nchi hii bwana ina filamu!

Nadhani ‘Part two’ ya Mzee Membe na Rostam itakuwa nzuri zaidi. Hii ‘Party one’ wamenikoroga sana. wote wawili wamenikoroga. Huyu tajiri kwa nini amtaje Membe, na kwa nini Mzee Membe hakutoa msimamo wake pale pale? Kweli mwaka 2019 umefika. Tuendelee kunywa mtori. Nyama tutazikuta chini.