Pendekezo la spika Ndugai kupangua majukumu sadc?

Siku tatu zijazo wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) wataanza rasmi vikao vya Mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo.

Ni mkutano unaofanyika baada ya hatua mbalimbali za mafanikio ndani ya mtangamano huo, hususani kusainiwa kwa itifaki za kibiashara, huduma, madini na utalii.

Kabla ya mkutano huo yamefanyika maonyesho ya wiki ya viwanda ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo. Pia kumekuwa na baraza la mawaziri wa SADC na ratiba nyinginezo.

Pamoja na ajenda nyingine za mkutano huo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai anaibua hoja ya kisiasa inayohitaji utekelezaji katika mkutano huo wa wakuu wa nchi inayoweza kubadili sura ya chombo hicho.

Anasema ni muda sahihi mkutano huo ukapitisha hoja ya kulifanya Jukwaa la Bunge la SADC (SADC-PF) kuwa Bunge rasmi la wabunge wa nchi 16 za SADC.

“Bunge la Tanzania lenye uwakilishi wa wabunge katika jukwaa hilo, limekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mtangamano wa SADC, limekuwa likijadili maslahi ya nchi wanachama ikiwamo utekelezaji wa itifaki ya bidhaa, madini, kilimo, utalii, sayansi na teknolojia.”

“Kwa kuona umuhimu wa jukwaa hilo, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kutetea jukwaa hili ili siku zijazo liweze kuwa Bunge kamili la kikanda. Ningependa kutoa wito kwa nchi nyingine wanachama, kuunga mkono hoja ya kuanzisha bunge litakalokuwa chombo madhubuti kuimarisha mtangamano huu,” anasema Ndugai.

Kwa mujibu wa Mdugai, tayari mapendekezo ya hoja hiyo yameanza kutolewa baada ya Rais John Magufuli Juni 28, 2019 kupokea ujumbe maalumu kutoka kwa Spika wa Bunge la Msumbiji na Rais wa Jukwaa hilo, unaopendekeza kulibadili kuwa Bunge Kamili la SADC lenye uwezo wa kukaa na kujadili mambi ya kutekelezwa na nchi wanachama.

“Ni matumaini yetu kwa mkutano unaokuja wa wakuu wa nchi za SADC pamoja na mambo mengine, utazingatia maoni haya kutoka kwa wabunge wa jukwaa la SADC,” anasema Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa.

Ndugai aliwasilisha ombi hilo Agosti 5, 2019 wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili ya washiriki wa maonyesho ya viwanda kwa nchi 16 za SADC.

Ikiwa pendekezo hilo litakubalaiwa SADC itaongeza chombo kingine cha maamuzi, na hivyo kuwapo uwezekano wa kupangua majukumu na hata muundo wale.

Majukumu ya SADC

Balozi Herbert Mrango anasema malengo ya kuanzishwa kwa SADC ni kuhamasisha ushirikiano wa shughuli za maendeleo ya kijamii, siasa na usalama miongoni mwa nchi wanachama ili kufanikisha maendeleo na ustawi wa watu.

“Katika maeneo ya ushirikiano ni pamoja na biashara, viwanda, huduma za kifedha na uwekezaji (TIFI), ni eneo muhimu SADC na malengo yake ni kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na uwekezaji miongoni mwa wanachama,” anasema Balozi Mrango.

Jumuiya hiyo tayari imeshasaini itifaki mbalimbali za ushirikiano ndani ya nchi wanachama. Nchi hizo zilisaini itifaki ya nishati, itifaki ya usafirishaji, mawasiliano na hali ya hewa na itifaki ya biashara mwaka 1996. Itifaki ya biashara ilianza utekelezaji wake mwaka 2000.

Aidha, nchi hizo zilisaini tena itifaki ya kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya mwaka 1998.

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Viwanda na ushindani katika Jumuiya hiyo, Dk Johansein Rutaihwa anasema SADC haina mamlaka ya kuamua jambo lolote kwa nchi inayokiuka makubaliano ya itifaki iliyosainiwa kwa mujibu wa mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo.

Kuhusu itifaki ya kibiashara, Dk Rutaihwa anasema suala la kuondoa vikwazo liko chini ya kila nchi mwanachama, ila SADC imekuwa ikifanya kazi ya kuratibu kurahisisha mazingira ya kibiashara.

“Pamoja na kusainiwa kwa itifaki hizo, bado haziwezi kutekelezeka hadi kila nchi mwanachama iridhie kupitia vikao vya Bunge la nchi yake, changamoto ni pale kila nchi inapotaka kulinda maslahi ya soko lake la ndani kwa hiyo bado kuna changamoto ya utayari wa kisiasa kila mmoja kuamua kuondoa vikwazo.”

Dk Rutaihwa anasema kwa utaratibu wa SADC utekelezaji wa itifaki husika utazingatia hatma ya nchi 13 kati ya 16 za jumuiya hiyo baada ya kuridhiwa na mabunge yao.