Polisi waua mtuhumiwa ujambazi

Thursday February 14 2019

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Serengeti. Tukio la polisi kumuua kwa kumpiga risasi Nyamhanga Matokore (45), mkazi wa Kijiji cha Nyamakendo, Wilaya ya Serengeti anayetuhumiwa kwa ujambazi limeibua sintofahamu kati ya jeshi hilo na ndugu wa marehemu.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki akisema mtuhumiwa huyo aliyeuawa alijaribu kutoroka muda mfupi baada ya kukabidhi silaha, ndugu wa marehemu wanalituhumu jeshi hilo kwa kumuua makusudi baada ya kumteremsha kutoka ndani ya gari lao wakiwa njiani kwenda kituo cha Polisi Mugumu.

Tukio hilo lilitokea kati ya saa 3:00 hadi 4:00 usiku wa Jumatatu wiki hii katika Kitongoji cha Nyamituruma, Kijiji cha Nyamakendo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alisema Matokore alikuwa kati ya watuhumiwa sugu wa ujambazi waliokuwa wakisakwa na polisi kwa kujihusisha na matukio kadhaa ya mauaji, ujambazi wa kutumia silaha na uwindaji haramu.

“Siku ya tukio askari polisi wakiongozana na viongozi wa kijiji walikwenda kwake usiku akawapeleka mpaka kwenye pagale alimokuwa amechimbia bunduki aina ya AK-47 ya Kichina iliyofungwa kwenye mfuko wa sandarusi ikiwa na magazini na risasi 62,” alisema.

Alisema baada ya kukabidhi alichukuliwa kwenda Kituo cha Polisi Mugumu kwa mahojiano, lakini wakiwa njiani aliruka kutoka ndani ya gari la polisi kwa lengo la kutoroka ndipo askari walifyatua risasi kwa lengo la kumtisha asimame, lakini moja ikampata na kufariki dunia akiwa njiani akikimbizwa hospitalini kuokoa maisha yake.

Kamanda Ndaki alisema haikuwa mara ya kwanza kwa mtuhumiwa huyo kukutwa na silaha kwani Januari Mosi, 2016 alitelekeza bunduki aina ya AK 47 yenye namba 065388 na risasi nne. Alitelekeza silaha hiyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Emmanuel Baru na kutoroka baada ya kubaini anatafutwa na polisi.

Kaka aituhumu polisi

Kaka wa marehemu, Simion Manguye, mkazi wa Kijiji cha Nyamakendo aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa mdogo wake aliuawa kwa kupigwa risasi muda mfupi baada ya kukabidhi silaha. “Waliamua kumuua makusudi baada ya kuwaacha viongozi wa serikali ya kijiji, haiwezekani mtu aliyefungwa pingu mikononi na miguuni aliruke kutoka ndani ya gari na kujaribu kutoroka,” alisema Manguye.

Uongozi wa kijiji

Akizungumzia tukio lililosababisha kifo cha Matokore, mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji alikiri kushirikiana na polisi mpaka marehemu akawakabidhi silaha, risasi na magazine mbili.

“Tulimkuta kwa Marwa Nyesuke na kwenda kwake na akakabidhi silaha hizo, alipomaliza tukaondoka hadi kituo kidogo cha polisi Machochwe wakasema tubaki sisi na mwenyekiti wa kitongoji hicho, tuliuliza kama watamwachia kwa kuwa alikuwa amekabidhi silaha wakakataa kuwa wanaenda naye kwa mahojiano,”alisema.

Alisema muda mfupi walisikia milio ya risasi, “baada ya muda polisi wakanipigia simu kuwa wamempiga risasi wakati anataka kutoroka na wanampeleka hospitali kwa ajili ya matibabu,”alisema.

Advertisement