Profesa Nyange: Usiingie kwenye kilimo ukiwaza kupata hasara

Thursday May 30 2019

Mratibu wa Mradi wa ASPIRES, Profesa David

Mratibu wa Mradi wa ASPIRES, Profesa David Nyange akizungumza kwenye Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililokuwa likijadili Kilimo na Maisha Yetu, jijini Dar es Salaam. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kuna baadhi ya watu huogopa kuingia katika sekta ya kilimo kwa kuhofia kupata hasara mara moja na kufikiri ni suala endelevu au baada ya kusikia watu waliowekeza wakilalamika kukumbwa na changamoto hiyo.

Lakini pia huenda alikutana na changamoto nyingi baada ya kufanya uzalishaji wa mazao yake jambo ambalo lilimuondolea hamu ya kuwekeza tena katika sekta ya kilimo kwa sababu hakuona faida ya kuingia kwenye mchakato huo.

Ila wadau wa sekta hiyo wanasema licha ya kilimo kuonekana kukabiliwa na changamoto mbalimbali hasa kwa upande wa wakulima mmoja mmoja lakini bado inazidi kukua tofauti na miaka iliyopita huku fursa nazo zikiongezeka.

Akichangia mada katika mjadala wa Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililobeba mada ya ‘Kilimo Maisha Yetu,’ mshauri wa sera za kilimo wa taasisi ya Aspires, Profesa Davis Nyange alianza kwa kusema, “kumekuwa na mawazo tofauti je sekta ya kilimo inasonga mbele au imebaki pale pale. Jibu ni kwamba sekta hii inasonga mbele licha ya kukabiliwa na changamoto.

Mjadala huo uliandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV na Radio One na ulidhaminiwa ni Benki ya NMB, CRDB, Aga Khan Foundation, Shirika la Chakula Duniani (Fao), taasisi ya Aspires na Mpango kuendeleza kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Saggot).

Jukwaa hilo lilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga; mwalikishi wa Fao nchini, Fred Kafeero; mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai na wadau wengine.

Advertisement

Katika mchango wake, Profesa Nyange anasema licha ya kilimo kusonga mbele bado kasi ya ukuaji wake haiendani na rasilimali zilizopo ikiwemo maji, watu, ardhi na kwamba bado kuna maeneo mengine kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi.

Anasema kuna dalili au viashiria vingi vinavyonyong’onyesha mageuzi ya sekta ya kilimo, huku akisema kwa uzoefu wake wa zaidi ya miaka 20 akiwa mtafiti amesafiri maeneo mbalimbali ya nchi, amejionea dalili chanya kwenye sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka iliyopita.

“Kwa siku za nyuma ukiona shamba zuri linalolimwa kisasa na kuendeshwa kwa teknolojia linaloendeshwa kibiashara mara nyingi linamilikiwa na mwekezaji wa nje. Lakini kwa mara ya kwanza tunaona mashamba hayo yaliyowekezwa kwa umakini yanayomilikiwa na wazawa,” anasema Profesa Nyange.

Profesa Nyange anafafanua kuwa sekta ya kilimo ni msingi wa uchumi na mageuzi ya viwanda kwa sababu huajiri takriban theluthi mbili ya asilimia 65.5 ya idadi ya Watanzania sanjari na kuchangia asilimia 29 ya pato la Taifa.

“Sekta ya kilimo ndio chanzo cha asilimia 65 ya malighafi ya viwanda. Kilimo ni muhimu kwa usalama wa chakula na lishe, inasaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kwa miaka 15 Tanzania imekuwa ikijitosheleza kwa chakula jambo ambalo si dogo na linapaswa kupongezwa,” anasema Profesa Nyange.

Profesa Nyange anasema kwa miaka yote hiyo Tanzania imekuwa ikizalisha ziada ya asilimia 20, lakini sehemu bado inakumbwa na changamoto hasa kwa watoto wa umri wa miaka miwili, tunasema zile siku 1000 kuanzia mimba inatungwa hadi anapofikisha miaka miwili.

Kwa mujibu wa Profesa Nyange, asilimia 34 ya watoto waliopo wana tatizo la udumavu, hata hivyo kiwango cha udumavu kimeshuka kutoka asilimia 42 hadi 34 kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, jambo ambalo ni jema huku akishauri kutiliwa mkazo kwenye uwekezaji wa chakula na lishe.

Fursa za Kilimo-Ongezeko la watu

Mtaalamu huyo wa utafiti na sera, anagusia fursa zinazopatikana katika kilimo akisema sasa mazingira yamebadilika na kwamba kuna fursa zaidi kuliko changamoto.

Anasema fursa hizo zinatokana na ongezeko la idadi ya watu mfano huku akisema umri wa Mtanzania sasa ni miaka 18 ambayo anaanza kujitegemea, kwa Afrika ni miaka 20 wakati Ulaya ni miaka 40.

“Tofauti iliyopo ni mtu wa kawaida kule Ulaya amefanya kazi zaidi ya miaka 15, ana uzoefu, anakopesheka na ameshajiandaa kustaafu. Lakini kwa Mtanzania wa kawaida ni miaka 18 ndio anaingia kuanzisha familia, kwa sababu hiyo kwa miaka 15 ijayo Tanzania itakuwa na mlipuko mkubwa wa idadi ya watu.

“Maana yake Mtanzania wa kawaida anajiandaa kuingia katika soko la ajira ikiwemo sekta ya kilimo na makisio ni kwamba miaka 15 ijayo tutafikia watu milioni 100, wengi wetu tuliomo humu ndani (ukumbini) hapa tutashuhudia wingi wa watu hawa.

Profesa Nyange anasema katika Afrika, Tanzania inashika nafasi ya tano kuwa na watu wengi, hiyo ni fursa kwa sababu kuna watu wengi watalishwa chakula, lakini kuna jukumu pia la kuhakikisha kila mtu anapata chakula.

Ukuaji wa miji

Profesa Nyange anasema fursa nyingine ni ukuaji wa miji, ambapo inakadiriwa kuwa ikifikapo 2025 zaidi ya nusu ya wakazi wa Afrika watakuwa wakiishi mijini na watakuwa wakitegemea soko kama chanzo cha chakula.

Katika mjadala huo, Kafeero aliahidi Fao kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo ya kitaaluma ili kupunguza umasikini wa kilimo. Alisema Serikali inalazimika kuwawezesha wakulima zaidi kwenye maarifa na ubunifu kupitia uwekezaji wa taasisi za elimu.

Kwa upande wake, Waziri Hasunga anasema kwamba sekta ya kilimo ilitengeneza asilimia 65.5 ya ajira za moja kwa moja kwa Watanzania huku akiongeza kwa kusema kuwa kilimo ndio sekta pekee ambayo ukitaka kuingia hauhitaji kufanyiwa usaili tofauti na sekta nyingine.

Advertisement