Purukushani DC, muuza madafu zaibua panga, bastola hadharani

Mtwara. Madai ya mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali kunusurika kukatwa panga na muuza madafu juzi, yameibua jipya baada ya Polisi mkoani Mtwara kudai alitoa bastola baada ya kutofautiana na mchuuzi huyo.

Hata hivyo, jeshi hilo limesema uchunguzi wa kina unaofanyika utaonyesha ukweli wa sakata hilo.

Taarifa iliyokuwa ikisambaa jana katika mitandao ya kijamii iliyothibitishwa na Machali inasimulia mkasa huo uliotokea juzi jioni katika kijiji cha Mikangaula wilayani humo.

Machali alipozungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema alisimama kijijini hapo kununua madafu na pia kukagua wafanyabiashara ndogo wenye vitambulisho na kuwahamasisha wasio navyo wajitokeze kununua, lakini mmoja wa wauza madafu aliyetambuliwa kwa jina la Seleman alianza kuikashifu Serikali akisema inawaibia wananchi.

“Ni kweli ilitokea (kutishiwa panga), nilienda kutoa taarifa jana kituo cha Polisi cha Mangaka hapa wilayani, kwa hiyo siwezi kuzungumzia kwa kina suala hilo hivi sasa kwa sababu liko chini ya uchunguzi,” alisema Machali.

Vitambulisho alivyosimama DC Machali kukagua ni vile alivyovitoa Rais John Magufuli, Desemba 10, 2018 kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ambavyo gharama yake ni Sh20,000 kila kimoja.

Hata hivyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chatanda alisema taarifa za awali alizozipata kutoka eneo la tukio zilidai baada ya DC Machali kutofautiana kauli na kijana huyo, alitoa bastola.

“Niko safarini Morogoro, hata hivyo taarifa za awali nilizozipata mimi ni kwamba, yeye (DC) alimtolea bastora huyo muuza madafu baada ya kupishana naye lugha,” alisema Kamanda Chatanda.

“Sasa mazingira ya kutoa hiyo bastora siyajui vizuri, mpigie msadizi wangu ofisini atakupa taarifa za kina.” Baada ya kupigiwa simu, Joseph Konyo anayekaimu nafasi ya Chatanda, alisema wamefungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema taarifa alizonazo zinaeleza kuwa baada ya purukushani, Machali aliwaita watendaji wa kijiji na kata, na akaamuru wawekwe ndani kwa kukosa nidhamu kwamba hawajahamasisha wafanyabiashara wa eneo lao kupata vitambulisho hivyo vya mjasiriamali.

“Sasa ilibidi mkuu wa mkoa aingilie kati, akawatoa. Akasema kama wana makosa wapelekwe kwenye mamlaka za kinidhamu siyo Polisi,” alisema Konyo.

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Bayakanwa alimuita mkuu huyo wa wilaya ofisini kwake kwa ajili ya mahojiano juu ya sakata hilo.

“Lakini siyo busara sisi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa linashughulikiwa kiutawala, sisi tunafanya uchunguzi wa tukio lile ili kubaini ukweli,” alisema mkuu huyo wa mkoa akisisitiza kuwa atalitolea ufafanuzi zaidi suala hilo baada ya kujiridhisha.

“Mimi mambo yangu ya kiutawala hayana hadhi ya kwenda kwenye media mpaka nitakapokuwa nimethibitisha ninachokitaka, sasa hivi sina cha kukuambia.”