Raha ya ufugaji ng’ombe huanzia kwa mtamba

Saturday November 17 2018

 

By Neema Mbisse, Mkulima mbunifu

Unafahamu kwamba inagharimu nini kumfanya mtamba kuzalisha maziwa? Na je unafuatilia maendeleo ya mtamba wako ili kuhakikisha mfumo wa ulishaji unakusaidia kufikia lengo hili?

Ikiwa jibu ni hapana, basi ni wakati wako kuingia ulingoni na kupata ufahamu. Wafugaji wengi wanaamini kuwa haigharimu chochote kuwafuga mitamba kwenye malisho.

Lakini kulisha mitamba uwandani hakutoshelezi kuwapatia virutubisho vinavyohitajika, na itakapofikia wakati wa kumpandisha mbegu, itakugharimu kuliko unavyodhani, tofauti na kama ungezingatia matunzo ya mtamba wako tangu mwanzo.

Mtamba aliyetunzwa vizuri anakuwa na afya nzuri na kuweza kuzaa katika umri wa miezi 24. Hii inamaanisha kuwa atazalisha maziwa mapema, kurudisha gharama na kumpatia faida mfugaji.

Wafugaji hawazingatii vigezo vyote vinavyochangia gharama za ufugaji wa mitamba wa maziwa. Gharama hizo ni pamoja na chakula cha virutubisho, majani (ikiwa ni pamoja na uwanda wa kuchungia), nguvu kazi, gharama za daktari wa mifugo, banda na malazi, ulishaji na maji.

Kwa kawaida wafugaji huondoa gharama hizo na kuzifanya kama ni sehemu ya ng’ombe, lakini inatakiwa kuhesabu gharama hizo peke yake. Kwa kiasi kikubwa, mafanikio au kutofanikiwa kwa mtamba hutokana na matunzo katika kipindi cha miezi miwili ya mwanzo tangu kuzaliwa.

Mazingira ya kuzalia ni muhimu sana, na kama inawezekana ng’ombe atengewe sehemu safi ya kumdondoshea ndama wakati wa kuzaa.

Umuhimu wa maziwa ya awali (dang’a)

Dang’a ni maziwa ya awali anayotoa ng’ombe baada ya kuzaa, hiki ni chakula muhimu kwa ndama. Dang’a ina virutubisho muhimu ambavyo hujenga mwili na kusaidia mmeng’enyo wa chakula tumboni, na kujenga kinga ya mwili.

Dang’a ni muhimu sana, na ni lazima ndama apewe kwa njia sahihi. Kinga ya mwili hutumika kwa haraka sana ndama anapozaliwa, hivyo ni muhimu kupatiwa maziwa ya awali kwa haraka ndani ya saa nne toka kuzaliwa.

Maziwa ya awali ni muhimu kwa kuwa pia hupunguza vifo vya ndama, na vifo kuongezeka kwa ndama ambao hawakupatiwa maziwa ya awali.

Unapofanya hesabu ni kiasi gani cha dang’a kinachohitajika kwa ndama, makadirio mazuri ni kumnywesha ndama asilimia nne hadi tano ya uzito wake. Kwa kawaida, inashauriwa ndama kupata dang’a lita mbili mara mbili kwa siku.

Siyo mnene sana, na wala hajakonda sana

Kumpatia ndama vyakula vya kutia nguvu ni muhimu. Ni lazima uhakikishe kuwa wana nguvu ya kutosha kukua, na kumfanya awe na joto la kutosha muda wote.

Uwezo wa mwili wa ndama kuvunjavunja kemikali mwilini na kuujenga mwili unakuwa ni mkubwa sana katika siku za mwanzo za maisha yake. Baridi na mazingira mapya husababisha uhitaji zaidi wa nguvu. Inashauriwa kulisha ndama kwa vyakula vyenye virutubisho vya hali ya juu, vyakula vya mwanzo vyenye protini kwa wingi (asilimia 21 ya protini).

Hii inaanza tangu ndama anapozaliwa mpaka wiki mbili baada ya kuachishwa kunyonya. Lisha chakula cha mwanzo (kiasi cha protini asilimia 18) kuanzia miezi mitatu mpaka sita, ikifuatiwa na chakula cha kukuza (protini asilimia 16) kilo tatu kila siku kwa miezi 12.

Kuanzia hapo na kuendelea, protini asilimia 17, inapendekezwa kiwango cha kilo 2.5 kwa siku. Kiasi kinaweza kubadilika kulingana na hali ya ndama.

Mtamba anatakiwa kukomaa na kufikia asilimia 90 ya uzito wake kabla ya kuzaa. Kuna uhusiano mkubwa kati

ya uzito na uzalishaji wa maziwa katika uzazi wa mwanzo. Kadri mtamba alivyo na uzito, ndivyo uzalishaji wa maziwa utakavyokuwa mzuri.

Kuwa makini

Kushinikiza ukuaji ili ndama wawe wanene hupunguza urefu wa maisha na uzalishaji. Kwa upande mwingine, mtamba mwenye umbo dogo atakuwa na uzalishaji mdogo na wanapata matatizo wanapozaa.

Miezi minne mpaka tisa, ni hatua muhimu sana ya ukuaji wa ndama. Ndama akinenepa sana, husababisha

upungufu wa chembe chembe za alveola ambazo zinahusika na uzalishaji wa maziwa.

Kupima ni kufahamu

Ni muhimu kufuatilia maendeleo ya mtamba wakati wote. Hii itasaidia kuepuka kupata mtamba mnene sana, au aliyekondeana. Jaribu kufuatilia uzito na urefu wa mtamba kila mwezi.

Baadhi ya wafugaji hawapimi, lakini wanawaelewa wanyama wao kwa kuwatazama, na kuweza kubaini kwa haraka kunapokuwa na tatizo.

Endapo mtamba anahitaji virutubisho, hakikisha anapata ipasavyo. Wasiwe wanene zaidi, lakini wawe katika hali nzuri. Kama ni gharama kufuga mitamba, ni gharama zaidi kutowatunza vizuri.

Makala haya yaliyoboreshwa ni kwa hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu. www.mkulimambunifu.org

Advertisement