Rais Magufuli kuzungumza na wafanyabiashara wadogo 1,000

Wafanyabiashara  ndogondogo (machinga) wakiwa wamepanga bidhaa  katikati ya  mtaa wa Congo, Dar es Salaam jana .Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Miezi mitano baada ya kukutana na wachimbaji wadogo wa madini, Rais John Magufuli anatarajia kuzungumza na takriban wafanyabiashara wadogo 1,000 Ijumaa ya wiki hii.Miezi mitano baada ya kukutana na wachimbaji wadogo wa madini, Rais John Magufuli anatarajia kuzungumza na takriban wafanyabiashara wadogo 1,000 Ijumaa ya wiki hii.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kila halmashauri (zipo 186) inatakiwa kuwaalika wafanyabiashara watano ambao watahudhuria mkutano huo utakaofanyika kuanzia saa 2:00 asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Kikwete, Ikulu jijini hapa.

Agizo hilo lililotolewa Mei 31, liliwataka wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara kuwasilisha majina hayo hadi Juni 2. “Orodha hiyo ionyeshe jina, aina ya biashara na namba ya simu ya mfanyabiashara husika, iwapo katika wilaya husika kuna mfanyabiashara ambaye pia ni kiongozi wa kisiasa au mtendaji wa Serikali wasisite kumpendekeza na wafanyabiashara hao wajigharamie,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Akizungumza Mwananchi kuhusu mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alisema ajenda kuu ni kusikiliza kero na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wanaowahudumia wananchi.

Kama alivyokutana na wachimbaji wadogo mapema Januari, Kandege alisema hii ni mara ya kwanza kukutana na kundi hilo, mara zote huzungumza na wenye viwanda vikubwa na wafanyabiashara wa kimataifa.

Alifafanua kuwa kazi ya kuwakusanya wafanyabiashara hao watano kutoka katika kila wilaya itaratibiwa na halmashauri husika chini ya uangalizi wa wakuu wa wilaya.

Kuhusu wanaotakiwa kualikwa, alisema wanaweza kuwa wenye maduka ya pembejeo, vyakula, nyumba za wageni na wengine wanaohudumia wananchi moja kwa moja ambao wataeleza changamoto wanazokabiliana nazo iwe kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) au ushirikiano duni wanaopata kutoka mamlaka zinazowahudumia.

Alipoulizwa, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye kama wanachama wake wamepata mwaliko huo alisema hana taarifa ila ana imani wataalikwa kama wasikilizaji.

Licha ya ajenda za mkutano huo kuwa za Serikali, alisema ana imani matokeo yatakuwa chanya kama ilivyotokea kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa madini.

“Ajenda ambazo huwa tunashirikishwa kuandaa ni iwapo kikao kitaitwa na Baraza la Wafanyabiashara la Taifa (TNBC), lakini mkutano huu ni wa Rais tunaweza kualikwa kama wasikilizaji,” alisema Simbeye.

Kuhusu kutoalikwa kwa TPSF, Kakunda alisema mkutano huo sio kwa ajili yao na kufafanua kuwa baada ya wafanyabiashara hao wadogo, ana imani kuwa baadaye Rais atazungumza na wa kada nyingine.

“Wizara tutakuwepo kusikiliza kinachojiri,” alisema Kakunda.

Kutokana na agizo hilo kuruhusu kualikwa kwa viongozi wa kisiasa au watendaji wa Serikali ambao ni wafanyabiashara wakubwa ndani ya halmashauri suala linaloweza kuleta mgongano wa maslahi, katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Ngemela Lubinga alisema kwa kuwa imetolewa na Serikali hawezi kuingilia utendaji.

“Rais na Serikali wanafanya kazi siku zote ndiyo maana alikutana na wachimbaji wadogo wa madini kusikiliza kero zao na kuzitatua kama ilani ya chama inavyoelekeza,” alisema.