Rais TLS aikosoa sheria mpya madini

Waziri wa Madini, Dotto Biteko

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kupitisha sheria mpya ya madini ya 2017, wadau wameikosoa wakisema ina changamoto nyingi kiutekelezaji.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema sheria hiyo imeleta manufaa makubwa tangu ilipoanza kutumika nchini.

Kwa upande wake, akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshala alisema licha ya uzuri wa sheria hiyo, inashindwa kutatua baadhi ya changamoto ikiwamo mikataba ya kampuni za madini ya zamani.

Alisema mikataba ya kampuni zilizokuwepo tangu miaka ya 1990 iliweka masharti ya kutokuvunjwa, hivyo akashauri Serikali ikae na kampuni hizo ili kutafuta suluhisho.

Hata hivyo, Biteko amesema sheria hiyo haina changamoto ya utekelezaji bali ni mtazamo wa watu wasioipenda wakihisi utapunguza wawekezaji.

“Wanaohisi hivyo wanakosea sana kwa sababu imeleta matokeo chanya zaidi, kwani kwa miaka 29 hatujawahi kusaini mikataba mikubwa ya madini ambayo uwekezaji wake ni wa Dola 100 milioni za Marekani,” alisema waziri huyo.